RC Mtambi akemea uvuvi haramu Mara

MARA-Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi tarehe 17 Februari, 2025 amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kwikuba, Kata ya Busambara, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na kuwakemea watu wote wanaojihusisha na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.
Mhe. Mtambi pia amewataka wananchi wote wa Mkoa wa Mara kuungana na kukemea uvuvi haramu na kutoa taarifa zinatazowezesha kuwakamata wanaojihusisha na uvuvi haramu katika ziwa Victoria ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Wanachokifanya ni kuhujumu misingi ya kiuchumi ya wananchi wote wanaotegemea Ziwa Victoria na mwisho wake tunajitengenezea umaskini na Serikali ya Mkoa wa Mara haitakubali hilo litokee,” amesema Mhe. Mtambi.

Mhe. Mtambi amesema Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara inajjiandaa kufanya operesheni maalum ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria hivi karibuni na itawachukulia hatua za kisheria watu wote wanakaojihusisha na uvuvi haramu watakaokamatwa katika operesheni hiyo.

Mhe. Mtambi amesema kwa sasa kuna tishio la kumalizika kwa samaki katika Ziwa Victoria kutokana na uvuvi haramu na matokeo yake upatikanaji wa samaki umepungua na kupelekea baadhi ya viwanda vilivyokuwepo kufungwa na kuwahamasisha wananchi kuwabaini, kuwakemea na kutoa taarifa kwa viongozi kuhusiana na watu wanaojihusisha na uvuvi haramu.

Mhe. Mtambi amewahakikishia wananchi kuwa uvuvi haramu usipokuwepo, samaki watarudi katika eneo hilo na itakuwa rahisi kuvishawishi uwekezaji wa viwanda vya samaki katika Mkoa wa Mara ambavyo vitanunua samaki pia kutoka eneo hilo.

Kanali Mtambi amesema kwa sasa Serikali inakamilisha upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege Musoma ambao unaweza kurahisisha usafirishaji wa samaki kutoka Mkoa wa Mara kwenda maeneo mengine nchini na nchi jirani na wavuvi kuwawezesha wavuvi kupata soko la uhakika.

“Uwekezaji huu wa Serikali hauna maana kama matumizi ya ndege zitakazokuja Musoma itakuwa ni kwa ajili ya kusafirisha abiria tu bila ya kuwepo na uhakika wa mizigo yoyote kutoka Mkoa wa Mara” amesema Mhe. Mtambi.

Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amewataka wananchi kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kufanya siasa za kiustarabu na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Mkoa wa Mara imejipanga kulinda amani na usalama wakati wote wa uchaguzi.

Mhe. Mtambi amewataka wanasiasa wa Mkoa wa Mara kujenga hoja, kuelezea sera za vyama vyao na kuacha kuwalazimisha wananchi kumchagua mgombea wanayemtaka wao.

Mhe. Mtambi ametumia pia fursa hiyo kumpongeza mbunge wa Musoma Vijijini Mhe. Prof. Sospeter Muhongo kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi wa eneo hilo maendeleo na hususan katika sekta za elimu, afya na kilimo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amesema Wilaya hiyo imeanzisha operesheni maalum ya kupambana na wavuvi haramu na wamejipanga kutokomeza tatizo hili ili kurejesha mazalia ya samaki katika aeneo hilo.

“Operesheni hii itawagusa wengi wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine na uvuvi haramu, tunawakaribisha wote wenye taarifa za watu wanaojihusisha na uvuvi haramu ili tuweze kuzifanyika kazi na kuwachukulia hatua za kisheria,” amesema Mhe. Chikoka.

Mhe. Chikoka amesema Wilaya ya Musoma kwa sasa imeamua kutoa kipaumbele zaidi katika shughuli za uwekezaji ikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji na uchimbaji wa madini ambazo ni shughuli muhimu za wananchi wa hiyo.

Mhe. Chikoka amesema katika mikopo ya vikundi vya wananwake, vijana na watu wenye ulemavu miradi ya uzalishaji mali imepewa kipaumbele ili kuwezesha uzalishaji mali katika maeneo makubwa ya kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news