MARA-Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi tarehe 17 Februari, 2025 ameshuhudia makabidhiano ya mradi wa uchimbaji wa visima saba vya kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa wa Mara na kumtaka mkandarasi wa mradi huo kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Mhe. Mtambi ametoa maagizo hayo katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika kijiji cha Kwikuba, Kata ya Busambara Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na kumtaka mkandarasi huyo na wengine wote ndani ya Mkoa wa Mara kutekeleza miradi yao kwa wakati.
“Serikali imekupatia zabuni hii baada ya kujiridhisha na uwezo wa kampuni yenu, sasa Mkoa wa Mara hatutaki visingizio katika utekelezaji wa mradi huu kama kuna changamoto tutaarifiwe mapema ili kuweza kuitatua,” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi anasema miradi ya maendeleo inalenga kutatua changamoto za wananchi na kuwataka wakandarasi wote wa Mkoa wa Mara kujitahidi kukamilisha miradai yao kwa wakati ili iweze kutumika na kutatua kero za wananchi wa Mkoa wa Mara.
Kanali Mtambi amesema mradi huu unaleta mwanga kuelekea maisha bora kwa wananchi wa Mkoa wa Mara ambapo mkulima anajua kwa uhakika analima lini na atavuna lini mazao yao na hivyo kuleta uhakika wa chakula. 

Mhe. Mtambi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Halmashauri zilizopata visima hivyo kutafuta masoko ya uhakika ya mazao yatakayolimwa katika mashamba yenye visima hivyo ili kuwahamasisha wakulima zaidi kushiriki kilimo cha umwagiliaji.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Mara Mhandisi Adelialidy Mwesiga amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Tume ya Taifa ya Uwagiliaji itachimba visima 1,300 nchi nzima katika awamu hii ya kwanza visima 70 vitachimbwa na kati ya hivyo visima saba vitachimbwa katika Mkoa wa Mara.
Mhandisi Mwesiga amesema katika Mkoa wa Mara visima hivyo vinategemewa kuchimbwa katika wilaya za Musoma, Bunda, Butiama na Tarime kisima kimoja kila Wilaya wakati katika Wilaya ya Serengeti vinatarajiwa kuchimbwa visima vitatu na visima hivyo vinatarajiwa kuwanufaisha wakulima zaidi ya 700 wa wilaya hizo.
“Katika Mkoa wa Mara mradi huu unategemewa kugharimu shilingi 244,033,440 na utatekelezwa na Mkandarasi mzawa na kusimamiwa na wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Uwagiliaji,” amesema Mhandisi Mwesiga.
Mhandishi Mwesiga amesitaja shughuli zitakazofanyika kuwa ni pamoja na utafiti wa upatikanaji wa maji katika maeneo yote saba, uchimbaji wa visima, uhakiki wa kujua kiasi cha maji kilichopatikana na ufungaji wa mifumo ya umwagiliaji.
Bwana Mwesiga amesema mfumo wa miundombinu ya umwagiliaji utakaotumika ni umwagiliaji kwa njia ya matone na mazao yatakayolimwa ni mbogamboga na mahindi na eneo zaidi ya ekari 40 zitamwagiliwa na kisima kimoja.
Kwa upande wake, Mkandarasi wa mradi huo Mubarak Twaha Ngwada wa Kampuni ya MNFM Construction amesema mradi huo wa kuchimba visima saba katika Mkoa wa Mara walitakiwa kukamilisha ndani ya miezi sita kwa mujibu wa mkataba wa zabuni yao iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uwagiliaji.
“Hata hivyo tunatarajia kuukamilisha mradi huu pamoja na kupima uwingi wa maji hayo ifikapo tarehe 4 Aprili, 2025 kwa visima vyote saba vya Mkoa wa Mara ili wananchi waendelee na shughuli za uzalishaji mali” ameahidi Bwana Ngwada.
Bwana Ngwada ameishukuru Serikali kwa kuiamini na kuipatia kampuni hiyo zabuni ya kutekeleza mradi huo na kuahidi kuutekeleza kwa ubora na ndani ya muda uliowekwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwikuba Bwana Kamunyilo Kubega Dominiko amesema tayari kijiji hicho kimepata eneo la kufanya kilimo cha umwagiliaji na kuunda kikundi cha wakulima wa kilimo cha umwagiliaji ambao watanufaika na mradi huo.
Bwana Dominiko amesema kwa kutumia maji ya kisima hicho wanakikundi wataweza kulima mazao mbalimbali ya muda mfupi ikiwemo mahindi na mbogamboga na kuboresha hali ya upatikanaji wa chakula katika eneo hilo.

Bwana Dominiko ameishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo ambao amesema ni mkombozi wa wakulima wadogo wadogo wa kijiji hicho ambao awali walikuwa wanalima kwa kutegemea mvua na hawakuwa na uhakika wa kuvuna mazao yao.