BoT yataja faida za Sera ya Fedha madhubuti

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa,Sera ya Fedha madhubuti ni msingi muhimu katika kufikia malengo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Hayo yamebainishwa leo Februari 25,2025 na Mchumi kutoka Kurugenzi ya Uchumi, Sera na Utafiti wa BoT,Dominick Mwita katika siku ya kwanza ya semina kwa waandishi wa Habari za uchumi kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam,Ruvuma na Zanzibar.

Semina hiyo ambayo inaendelea katika tawi la BoT mkoani Mtwara, Mchumi huyo alikuwa akielezea kuhusu maana ya Sera ya Fedha inayotumia Riba ya Benki Kuu (CBR).

“Kutokana na changamoto zilizoambatana na mfumo wa sera ya fedha unaotumia ujazi wa fedha, kuanzia Januari 2024, Benki Kuu imehamia katika mfumo mpya wa sera ya fedha unaolenga riba.

“Mfumo unaotumia riba ndio unaotumiwa na nchi nyingi duniani na una faida za ziada ukilinganisha na mfumo unaotumia ujazi wa fedha.”

Mchumi huyo amezitaja faida hizo kuwa, ni mabadiliko ya riba ambapo yanaakisi kwa uwazi zaidi mabadiliko ya mahitaji ya ukwasi na uwepo wa ukwasi sokoni.

Pia, amesema wananchi wanaelewa malengo ya riba kwa urahisi na vizuri zaidi kuliko malengo ya ujazi.

Amesema, vilevile kuhamia mfumo wa sera ya fedha unaotumia riba ni hatua moja katika kutekeleza makubaliano ya kurahisisha sera za fedha katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mchumi huyo ameongeza kuwa,mfumo huu mpya wa utekelezaji wa Sera ya Fedha hutumia Riba ya Benki Kuu (CBR) ili kuhakikisha mfumuko wa bei ni tulivu na unabakia katika kiwango kidogo.

"Katika mfumo mpya,riba ya mikopo ya siku saba baina ya mabenki (IBCMR) hutumika kama kiashiria cha utendaji cha Sera ya fedha ya Benki Kuu, tofauti na awali ambapo Benki Kuu ilikuwa inadhibiti fedha za msingi."

Kwa mujibu wa Mchumi huyo, Sera ya Fedha hujumuisha maamuzi na hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu ili kupunguza au kuongeza ujazi wa fedha kufikia malengo ya kiuchumi.

Amesema, mafanikio ya ukuaji wa uchumi hutegemea usimamizi bora unaokwenda sambamba na utekelezaji wa sera mbalimbali ikiwa ni pamoja Sera ya Fedha (Monetary Policy).

Sera ya kibajeti (fiscal policy),sera za kisekta akitolea mfano sera ya kilimo, biashara, viwanda na nyinginezo.

"Sera hizi za kusimamia uchumi hubadilika kulingana na maendeleo na mahitaji ya uchumi husika."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news