TANGA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa,Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza kutoa ruzuku kwenye miradi ya nishati ya gesi ya kupikia, majiko ya gesi na majiko ya umeme ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuhamasisha na kurahisisha upatikanaji wa nishati safi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua usambazaji wa Nishati safi ya kupikia kwa Mkoa wa Tanga katika viwanja vya CCM Jitegemee kabla ya kuwahutubia wananchi wa Muheza mkoani humo tarehe 27 Februari, 2025.


Aidha,Rais Dkt.Samia amesema Serikali itaendelea kutunga sera zitakazoimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa bei nafuu na kwa urahisi ili kuimarisha uıstawi wa wananchi na kulinda mazingira.
Katika hatua nyingine,Rais Dkt. Samia amefungua rasmi kiwanda cha Saruji na Chokaa cha Maweni Limestone katika Jiji la Tanga, uwekezaji unaoendana na dhamira ya Serikali ya kurejesha hadhi ya Mkoa wa Tanga kama mkoa wa viwanda.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa uamuzi wa kampuni ya Maweni Limestone kupanua uwekezaji wake nchini ni ishara ya imani ya wawekezaji kwa sera za uwekezaji, mazingira ya biashara na rasilimali watu nchini Tanzania.

Vilevile,Rais Dkt. Samia ameweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Maji wa Tanga-Horohoro unaohusisha ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomnita 91.9.
Akizungumza na wananchi katika Stendi ya Mabasi Mkinga Rais Dkt. Samia amesema mradi huo utawahakikishia maji safi na salama wananchi takriban 57,000 katika Vijiji 37 katika Wilaya ya Mkinga na Wilaya ya Tanga.
Matukio hayo yamefanyika ikiwa ni siku ya 5 ya ziara ya Rais Dkt. Samia katika Mkoa wa Tanga.
Februari 28, 2025, Rais Dkt Samia anatarajia kuzungumza na wakazi wa Mkoa wa Tanga katika Mkutano wa Hadhara utakaofanyika katika Uwanja wa Mkwakwani katika Jiji la Tanga.