ZANZIBAR-Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan amewataka Masheha kuwa na ushirikiano katika kuhakikisha wanayaimarisha mabaraza ya vijana katika Shehia wanazoziongoza.

Amesema, Masheha si viongozi tu wa wananchi bali ni walezi wa vijana hivyo kutumia busara na hekima zao kuhakikisha vijana wanajiunga na kuwa na wanachama wa Baraza la Vijana Zanzibar ili kupata fursa zitolewazo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na taasisi binafsi kupitia Baraza la Vijana Zanzibar.
"Kujiunga na Baraza la Vijana Zanzibar kwa kijana kuna faida na fursa azipatazo kijana akiwa mwanachama ikiwa ni pamoja na kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha kujiajiri na Kuajirika,"alisema Katibu huyo.
Aidha,amewaomba Masheha hao kushirikiana na Baraza la Vijana Zanzibar kutafuta njia sahihi ya kutatua changamoto za Vijana ikiwa ni pamoja na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya udhalilishaji.

Akizungumza Sheha wa Shehia ya Mchina,Bi. Zam Zam Ali Rijali ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapatia Vijana kuwapatia Miradi itakayowawezesha kujikwamua Kimaisha kupitia Shehia zao.

Baraza la Vijana Zanzibar kupitia Kikao hicho limeadhimia kuandaa utaratibu wa Kuzungumza na Masheha kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kupeana mrejesho na kuyaimarisha mabaraza.