Serikali yazidi kuwaheshimisha wanawake nchini

ZANZIBAR-Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ndugu Abeida Rashid Abdallah amesaini Mpango wa Taifa wa kushughulikia Utekelezaji wa Ajenda ya Masuala ya Wanawake kuhusu Amani na Usalama ulioandaliwa mahsusi kwa ajili ya kutekeleza Azimio Na:1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,ndugu Abeida Rashid Abdallah akitia Saini Mpango wa Taifa wa kushughulikia Utekelezazi wa Agenda ya Wanawake, kuhusu Amani na Usalama, hatua ya utiaji Saini imefanyika ofisini kwake Kinazini Unguja, siku ya Febuari 3,2025. (Picha na Maryam Seif).

Hafla ya utiaji saini imefanyika jana ofisini kwake Kinazini Unguja, amesema mpango huo ni heshima kwa Tanzania kwani imeonesha wazi kukubali na kutekeleza Azimio hilo la Umoja wa Mataifa la kuhakikisha Wanawake wanakua katika amani na usalama wakati wote.

Amefahamisha kwamba, Azimio hilo lilipitishwa tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 2000, kwa lengo la kuhimiza umuhimu wa nafasi ya wanawake katika kuzuia na kutatua mizozo, mashauriano ya amani, ujenzi wa amani, ulinzi wa amani, hatua za usaidizi wa kibinadamu na ujenzi baada ya mizozo na kusisitiza umuhimu wa ushiriki sawa katika uendelezaji wa amani na usalama duniani.
Ameeleza kuwa, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Tanzania Bara kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo, Sekta zingine za Umma na Binafsi wameshirikiana katika kuandaa mpango huo ili kuleta ufanisi katika utekelezaji.

“Katika uwandaji wa Mpango huo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia ,Wazee na Watoto ndio Waratibu wakuu waliosimamia Mpango huo, lakini sekta zingine zinazoshughulika na masuala ya wanawake zimehusihwa kwa ajili ya kutoa maoni yao,”amesema Katibu Mkuu huyo.
Naye Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,ndugu Siti Abbas Ali amesema, mpango huo utasaidia katika kuongeza nguvu ya utetezi wa masuala ya wanawake ili wabaki salama katika harakati zao zakujitafutia kipato.

Amefahamisha kwamba, mbali na suala la amani, Mpango huo pia unaelekeza namna ya kulinda amani na kuleta suluhisho wakati wa migogoro kwani mwanamke akikosa amani hatoweza kufanya shughuli zake za kujiletea maendeleo.
Akizungumza Afisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, ndugu Timotheo Gabriel Mgonja amesema, mchakato wa kuandaa mpango huo ulianza mwaka 2020 na sasa upo katika hatua za mwisho na unatarajiwa kuzinduliwa mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news