DODOMA-Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuwa uwanja wa Michezo unaotarajiwa kujengwa jijini Dodoma utagharimu shilingi Bilioni 352 ambazo ni fedha kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Prof. Kabudi ameyasema hayo leo Februari 13, 2025 jijini Dodoma wakati wa hafla ya Utiaji Saini kati ya Wizara hiyo chini ya Katibu Mkuu wake Ndg. Gerson Msigwa na Kampuni ya Limonta SPA kutoka nchini Italia.
Prof. Kabudi ameeleza kuwa, ujenzi wa uwanja huo utatumia muda wa miezi 24 na utakuwa na uwezo wa kubeba watu 32,000.
Aidha, Waziri Kabudi amesema kuwa Serikali inaendelea na ukarabati wa miundombinu mingine ya michezo kama vile ukarabati wa Uwanja wa Mkapa ambao umefikia asilia 75 na uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi ameeleza kuwa, Mradi huo utakuwa na fursa lukuki kwa wakazi wa Dodoma ikiwemo Ajira na biashara pamoja na kuwataka wadau mbalimbali Kutengeneza mazingira wezeshi ya huduma muhimu kama vile Umeme, Maji, barabara na mawasiliano vitakavyowezesha mkandarasi kuendana na kasi inayotakiwa.
