KATIKA kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kiasi cha Sh.Trilioni 1.3 kimetumika kufanya maboresho makubwa kwenye miundombinu ya kutolea huduma za afya, vifaa na vifaa tiba, dawa na ubora wa utoaji wa huduma za afya ya msingi nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume ameyasema hayo leo Februari 19, 2025 alipokuwa akizungumzia mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita katika utoaji wa huduma za afya ngazi ya msingi nchini.
Amesema fedha hizo zimetumika kufanya uwekezaji katika afya msingi na kuchangia ongezeko la miundombinu ambapo hadi sasa kuna zahanati 6163, vituo vya afya 932 na hospitali za Wilaya 188.
“Mpaka sasa kuna hospitali mpya za Wilaya 129 ambazo zimejengwa kwenye maeneo ya pembezoni, hospitali kongwe 48 zimeboreshwa, vituo vya kutolea huduma za afya 367 vyenye uwezo wa kufanya upasuaji, kuongeza, damu,” amesema.
Dkt. Mfaume amesema uwekezaji huo umesaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto kutoka vizazi hai 556 hadi 104 katika kila vizazi hai 1000.
Pia, amesema katika maeneo ya vijijini kulikuwa na changamoto kubwa ya kupeleka watumishi wa afya na ilitokana na kutokuwa na nyumba za kuishi lakini mpaka sasa Serikali imejenga nyumba 270 kwa ajili yao.
Pamoja na hayo, amesema Serikali imejenga majengo ya kutolea huduma za dharura 86, magari ya kubebea wagonjwa 382 yamesambazwa kwenye halmashauri zote huku kwa kipindi hicho watumishi 25,936 wameajiriwa.