MANYARA-Kocha Msaidizi wa Simba Sports Club, Darian Wilken amesema maandalizi ya mchezo wa leowa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Fountain Gate FC utakaopigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa yamekamilika.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg8nGO5rHICePQm-JsHVsvUDQwGAGss1KtrTTSUmz7Pw8e-nAbn9d6BDhTIV2-UBqsMmoP6mzqFdE795lsh9ynLESZykDhyphenhyphen7MUVmHOfepMWz47NxFbtjBoUyyamsz09y1T26KO5GZR8oq4Naz1gVmFzLQL8_h-hsMFerWHpV910gsvHbswjdIoB_R9vJ22k/s16000/1001171827.jpg)
Wilken ameongeza kuwa, mzunguko wa pili wa ligi ni mgumu na kila timu imejipanga kuhakikisha inafanya vizuri hasa ikiwa nyumbani,lakini wamejiandaa kupambana na changamoto yoyote itakayojitokeza.
“Maandalizi yamekamilika, kikosi kimefika leo Manyara na jioni kitafanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo wa kesho ambao tunaamini utakuwa mgumu,” amesema Wilken.
Kwa upande wake nahodha wa timu Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema, kwa upande wao wachezaji wapo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha alama tatu zinapatikana.
“Malengo yetu kwenye kila mchezo ni kuhakikisha tunapata alama tatu, kwetu kila mechi ni fainali na tupo tayari kupambana hadi mwisho ili kufanikisha hilo,” amesema Zimbwe Jr.