NA DIRAMAKINI
SIMBA Sports Club (Simba SC) ya jijini Dar es Salaam imerejea kwa kishindo katika kilele cha msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, baada ya kuichapa Tabora United FC mabao 3-0.
Ushindi huo umewawezesha Wekundu hao wa Msimbazi kuwaporomosha watani zao kileleni hapo baada ya kudumu kwa saa 24.
Mtanange huo kati ya Simba SC na Tabora United FC umepigwa leo Februari 2,2025 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.
Simba SC walianza mchezo huo kwa kasi huku wakifika mara nyingi langoni mwa Tabora United FC ingawa walikosa ufanisi wa kumalizia nafasi walizopata.
Leonel Ateba aliwapatia Simba SC bao la kwanza dakika ya 12 kwa shuti kali nje ya 18 baada ya kupokea pasi safi ya Elie Mpanzu.
Vilevile,Ateba alitupia bao la pili kwa mkwaju wa penati dakika ya 34 baada ya Mpanzu kufanyiwa madhambi ndani ya 18 na mlinzi wa Tabora United FC.
Simba SC katika kipindi cha pili aaliongeza kasi ya kutafuta mabao zaidi huku Tabora United FC nao wakifika mara kadhaa langoni mwa Simba,lakini walikuwa imara kuwadhibiti.
Shomari Kapombe aliipatia Simba SC bao la tatu dakika ya 65 kwa shuti la chini chini la mguu wa kushoto baada ya kumalizia pasi safi iliyopigwa na Ateba.
Kwa matokeo hayo,Simba SC imefikisha alama 43 baada ya mechi 16 huku Tabora United ikisalia nafasi ya tano kwa alama 25 baada ya mechi 16.
Tags
Habari
Leonel Ateba
Ligi Kuu ya NBC
Michezo
Shomari Kapombe
Simba Sports Club
Tabora United FC
Yanga SC