LINDI-Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids amesema baada ya mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji kuahirishwa wikiendi iliyopita kikosi chake kimepata muda mrefu wa kujiandaa kabla ya leo kukutana na Namungo FC katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Fadlu amesema kabla ya kikosi kufika Ruangwa kilipata muda wa kufanya mazoezi kabla ya kuivaa Namungo leo.
Akizungumzia mchezo wenyewe, Fadlu amesema utakuwa mgumu hasa baada ya wapinzani kuzidi kuimarika huku akiweka wazi uwepo wa kocha mzoefu, Juma Mgunda utazidi kuifanya mechi kuwa ya ushindani.
Fadlu ameongeza kuwa, lengo la kwanza kwenye mchezo wa leo ni kupata alama tatu na la pili ni kuhakikisha wanapata mabao mengi ambayo yatatawanyika kila eneo bila kutegemea mchezaji mmoja.
“Mpango wetu ni kuhakikisha magoli yanapatikana pande zote ndio maana unaona walinzi Shomari Kapombe na Mohamed Hussein wanahusika kwenye kufunga na kutoa ‘asisti’ viungo na washambuliaji ni jukumu lao pia lakini hatutaki kuwapa presha wachezaji wetu,” amesema Fadlu.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia, David Kameta ‘Duchu’ amesema wanategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Namungo,lakini wamejipanga kuhakikisha wanashinda na kupata alama tatu ugenini.
Duchu ameongeza kuwa,wamekuwa wakipata wakati mgumu wanapokutana na Namungo katika uwanja wa Majaliwa lakini wapo tayari kupambana hadi mwisho ili kufanikisha malengo.
“Mchezo dhidi ya Namungo haujawahi kuwa rahisi, katika miaka miwili iliyopita hatujapata ushindi hapa lakini tumekuja kamili kuhakikisha tunashinda,” amesema Duchu.