SONGWE-Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limepongezwa kwa kasi kubwa ya maendeleo lililoyapata kwa miaka michache iliyopita.
Hayo yamesemwa leo Februari 22,2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,ndugu Msafiri Mbibo kwenye hotuba yake wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa STAMICO unaofanyika kwenye Mgodi wa Kiwira uliopo Wilaya ya Ileje mkoani Songwe.
"Kasi ya maendeleo serikali inayoiona ndani ya STAMICO kwa miaka michache iliyopita hadi sasa ni ishara kuwa kuna mwanga siku zijazo."
Amepongeza mshikamano uliopo kati ya menejimenti na watendaji wote ndani ya Shirika ambao ameuelezea kuwa ni msingi wa mafanikio yaliyofikiwa.
"Mafanikio haya yanahitaji kupongezwa na nitoe rai kwa watendaji wote kufanya kazi kwa bidii,uadilifu, uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja na kwa pamoja ili kuongeza kasi ya kukua kwa mapato ya Shirika,"alisema ndugu Mbibo na kuongeza.

Ametoa ushauri kwa shirika kuongeza kasi na kuweka mikakati ya kuchimba madini ya aina mbalimbali kwa kutumia leseni zake au kukaribisha wawekezaji ili Tanzania iwe ni kivutio duniani kote kwenye sekta hii.
Amewapa changamoto wajumbe wa Baraza kuwa wabunifu na kuwashirikisha wafanya kazi wote wa Shirika ili watoe mawazo yao kabla vyombo vya juu havijafanya maamuzi.
Aidha,amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO,Dkt.Venance Mwasse kwa maono yake makubwa yaliyobadilisha Shirika na hasa Mgodi wa Kiwira kutoka utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini hadi kuwa Shirika linalojitegemea kwa asilimia 100 kwa fedha za kujiendesha na kutoa gawio serikalini.

Ametoa rai kwa menejimenti kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi kwa wakati.
Awali,Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO wakati akitoa salamu za Shirika kwa mgeni rasmi amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na watendaji wote kwa uadilifu na uwajibikaji wa pamoja.
"Nitumie nafasi hii kuishukuru Wizara ya Madini na serikali yote kwa ujumla inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miongozo mbalimbali ya kisera na fedha za maendeleo kwenye miradi ya kimkakati.
Amesema,shirika linatekeleza miradi mbalimbali kama vile uchorongaji kwenye migodi mikubwa hapa nchini,huduma ya uchorongaji kwa wachimbaji wadogo pamoja na mradi wa kuzalisha nishati safi na salama ya kupikia ya Rafiki Briquettes ambayo inatumiwa kwa wingi kwenye taasisi za umma kama vile Jeshi la Magereza.
