Tanzania kunufaika na uchimbaji madini ya Niobium

IMEELEZWA kwamba Madini ya Niobium ni moja ya madini adimu na muhimu katika sekta ya teknolojia, ujenzi na matumizi ya viwandani hasa katika utengenezaji wa vifaa vya superalloys vinavyotumika katika anga za juu, magari ya kisasa pamoja vifaa vinavyostahimili joto kali.
Vilevile kutengeza sumaku kwenye mota za magari ya umeme, betri za magari ya mseto na umeme;na vitu vingine mbalimbali vya umeme.

Sambamba na matumizi katika nyanja za sayansi na teknolojia pia madini ya Niobium hutumika katika mitambo ya uchorongaji katika tafiti na uchakataji wa mafuta na gesi.

Akijibu swali Bungeni, Oktoba 31,2024 Naibu Waziri wa madini Dkt. Steven Kiruswa alieleza kuwa Tanzania inatarajia kuanza uzalishaji wa madini ya Niobium kupitia mradi wa Mamba Minerals Corporation Limited (MML), kampuni ya ubia katika ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Hisa asilimia 16% na kampuni ya Peak Resources Ngualla Company (PRNG) ya nchini Australia yenye asiliamia 84%.

MML ni kampuni inayomilika leseni kubwa ya uchimbaji (Special Mining licence- SML) wa Madini Mkakati (Critical Minerals) yenye jina la Rare Earth Elements. Mradi upo kijiji cha Ngwala, Mkoani Songwe, takribani km 1000 kutokea Dar es Salaam na km 150 kutokea Mbeya Mjini; Uhai wa mgodi unakadiriwa kuwa miaka 24.

Pamoja na mambo mengine , katika mahojioano na kituo cha televisheni cha CNBC Africa wakati wa mkutano wa Indaba Mining 2024 nchini Afrika Kusini, Dkt. Kiruswa alielezea kuhusu uwepo wa madini muhimu yaliyopo Tanzania yakiwemo madini ya Niobium pamoja na mikakati ya uwekezaji katika maeneo yenye rasilimali hizo.

Madini ya Niobium yatakayochimbwa yataongezewa thamani nchini kwa kuchanganywa na madini ya chuma ili kuzalisha ferroniobium, bidhaa inayohitajika katika masoko ya nchi za Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini.

Tanzania itafaidika kwa namna mbalimbali katika uchimbaji wa madini ya Niobium ikiwemo Kuongeza Mapato ya Serikali, kuimarisha Sekta ya Viwanda na Teknolojia, Kuhamasisha Uwekezaji wa Ndani na Nje.

Nchi zinazoongoza kwa uchimbaji wa Niobium Afrika ni pamoja na Msumbiji ambayo ina mradi wa Mozambique Niobium Project, Rwanda kupitia uzalishaji wa madini ya tantalite na cobalt ambayo uambatana na Niobium, nchi nyingine ni Afrika Kusini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news