DAR-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Vietnam, Mhe. Le Thi Thu Hang kuhusu umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili.
Wakizungumza katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam, Februari 28, 2025, Waziri Kombo amesema anatambua ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Viet Nam na anaamini kuwa bado yapo maeneo mengi muhimu ambayo nchi hizi mbili zinaweza kuboresha ushirikiano hususan katika sekta ya biashara, kilimo na uwekezaji.

Katika kilimo, Mhe. Kombo ameongeza kuwa Viet Nam ni nchi ambayo iko vizuri katika kilimo cha umwagiliaji na uhifadhi wa mazao, eneo ambalo Tanzania inaendelea kujinoa katika ujuzi huo utakaosaidia wakulima kulima kwa kutotegemea misimu ya mvua ambayo kwa sasa imeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi lakini pia kuweza kuhifadhi mazao yao kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mhe Hang ameafiki kupanua wigo wa ushirikiano katika maeneo hayo na kuomba ushirikiano kutoka kwa Serikali ya Tanzania pale ambapo ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Vietnam utakapokuja kuangalia mazingira na mahitaji ya uwekezaji na biashara.