TLP watibuana, wanachama 21 wafukuzwa








DAR-Mgogoro mkubwa umeibuka ndani ya Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), kufuatia mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Februari 2 , 2025 katika Ukumbi wa Mrina Hotel Tip Top Manzese jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo, inadaiwa kuwa ulifanyika bila kufuata utaratibu wa kikatiba na kutokuwa na uwazi, umeibua malalamiko makubwa kutoka kwa wanachama wa chama hicho, huku wakituhumu kuundwa kwa uongozi wa kinyemela na kwa manufaa ya watu wachache.

Katibu Mwenezi wa TLP Taifa, Geoffrey Stephen Paulo, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari, akieleza kwamba baada ya mkutano mkuu, wamepokea malalamiko kutoka kwa wanachama na wajumbe wa mkutano mkuu pamoja na halmashauri kuu ya chama hicho.

“Tumepokea malalamiko kutoka kwa wanachama wa TLP wakilalamikia kukiukwa kwa utaratibu wa kuitishwa kwa mkutano mkuu.

Wajumbe halali wakiwa wameachwa mikoani bila taarifa, na badala yake watu wasiokuwa wanachama walialikwa na kuvalishwa T-shirt za chama.”

Kwa mujibu wa Paulo, mkutano huo ulijumuisha wajumbe feki waliokusanywa mtaani na kupewa mavazi ya chama, jambo ambalo limezua mivutano kubwa ndani ya chama hicho.

Hali hii iliwafanya wanachama wengi kulalamika kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki na haukufuata katiba ya chama.

Paulo aliongeza kuwa chama kimechukua hatua ya kuwasilisha malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, na pia tayari wameanzisha mchakato wa kumpeleka Kaimu Mwenyekiti, Hamad Mkadamu, na Katibu wake, Richard Lyimo mahakamani kwa tuhuma za ukiukwaji wa katiba ya chama.

Katika mkutano huo, Richard Lyimo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa TLP kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, akiwa mgombea pekee katika nafasi hiyo.

Hata hivyo, uchaguzi huu haukukubalika kwa baadhi ya wanachama ambao walidai kuwa mchakato wa uchaguzi ulikuwa wa kinyemela.

Katika mkutano huo, pia alichaguliwa Johari Hamis kuwa Makamu Mwenyekiti Bara, ambaye pia alikuwa mgombea pekee katika nafasi hiyo.

Mkutano huo pia uliridhia kwa kauli moja kuwafukuza wanachama 21, wakiwemo viongozi wa chama, kwa tuhuma za kujaribu kuandaa mikutano ya kinyemela ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi kufuatia kifo cha Mwenyekiti wa zamani, Agustino Mrema, mwaka 2022.

Wanachama na viongozi waliotimuliwa ni pamoja na;

■Dominata Rwechangura (Makamu Mwenyekiti Bara)
■Ivan Maganza (Mwenyekiti wa Vijana Taifa)
■Mariam Kassin
■Riziki Nganga
■Stanley Ndumagoba
■Mary Mwaipopo
■Mohamed Mwinyi
■Laurian Kazimiri
■Nataria Shirima
■Kinanzaro Mwanga
■Godfrey Stivin
■Rashid Amiri
■Twaha Hassan
■Tunu Kizigo
■Damari Richard
■Hamad Alawi
■Mohamed Hemed
■Mariam Hamis
■Mussa Fundi
■Mwajuma Mussa
■Osward Nyoni

Wanachama hawa walifukuzwa uanachama kwa kile kinachodaiwa kuwa ni jaribio la kupinga uongozi halali wa chama na kufanya mikutano ya siri. Hali hii imesababisha mgogoro mkubwa ndani ya chama, huku wakihoji uhalali wa vikao vya chama na mchakato wa uchaguzi.

Wakati malalamiko yanaendelea, Msemaji wa chama hicho Geoffrey Stephen Paulo ambaye ni miongoni mwa waliotimuliwa alisisitiza kuwa chama kimechukua hatua za kisheria kupinga uhalali wa mkutano huo, na kwamba wanachama wa mikoa mbalimbali wamewasilisha maandiko rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, wakilalamikia ukiukwaji wa katiba. 

“Tunakusudia kuwaburuza mahakamani kaimu mwenyekiti na katibu wake walioitisha mkutano huo waende kueleza mahakama namna walivyokiuka katiba ya chama na kufanya uchaguzi usio halali.”

Aliongeza kwamba wanachama wanatarajia mahakama itachukua hatua stahiki na kuzuia uongozi wa Kaimu Mwenyekiti na Katibu wake hadi kesi hiyo itakaposikilizwa.

Mgogoro huu unaendelea kuwa chanzo cha wasiwasi kwa wanachama wa TLP, huku wengi wao wakieleza kuwa chama kinahitaji kurekebisha mchakato wake wa uchaguzi ili kuepuka migawanyiko zaidi.

Wanachama wengi wanatamani kuona TLP ikiendelea kuwa chama cha siasa chenye umoja na utulivu, lakini wanadai kuwa hatua ya uongozi wa sasa ni kikwazo kwa maendeleo ya chama. 

“Tunaomba wanachama na watanzania wote wanaoitakia mema chama cha TLP wawe watulivu wakati huu ambapo tunasubiria majibu ya rufaa kutoka kwa msajili wa vyama vya siasa na utaratibu wa mahakama kukamilika,”amesema Paulo.

Kwa sasa, TLP inakabiliwa na changamoto kubwa ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na mivutano ya ndani ya chama, na iwapo mgogoro huu hautashughulikiwa kwa haraka, huenda ukaleta madhara makubwa kwa uongozi na umoja wa chama hicho katika siku zijazo.

Wanachama wanatarajia kuona hatua za haraka zitachukuliwa na vyombo vya sheria hasa mahakama na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ili kurejesha amani na utulivu ndani ya chama hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news