Tuendelee kutumia mifumo ya malipo kidijitali kuimarisha uchumi,usalama huduma za kifedha-BoT

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi kuendelea kutumia mifumo ya malipo kidijitali ili kuimarisha uchumi, usalama na huduma za kifedha kwa ustawi wao na Taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa leo Februari 27,2025 na Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Idara ya Mifumo ya Malipo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Kidee Mshihiri wakati akiwasilisha mada katika semina kwa waandishi wa habari za uchumi,biashara na masoko ya fedha inayoendeshwa na BoT katika tawi lake mkoani Mtwara.

Katika wasilisho lake la malipo ya kidigitali kwa bidhaa na huduma,Mshihiri amesema kuwa,pia mifumo hiyo licha ya kurahisisha huduma imekuwa ikisaidia Serikali kukusanya kodi kwa wakati.

"Kwa hiyo wananchi tuendelee kutumia mifumo ya kidijitali katika kufanya malipo, manunuzi na huduma nyingine kupunguza fiscal cash. Hii ni njia salama zaidi, pia matumizi ya kadi yanasaidia usalama wako.

"Na, wananchi waendee kuwa kidijitali kwa sababu miaka minne, mitano ijayo tunataka kwenda kwenye cashless economy."

Amesema, matumizi ya mifumo ya malipo ikiwemo Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Papo (TIPS) ni pamoja na kuwezesha ushirikiano kati ya watoa huduma za fedha za kidijitali.

Pia, mfumo huo unaongeza ufanisi wa mifumo ya malipo ya thamani ndogo ambapo uchakataji huwa unafanyika papo kwa papo.

Faida nyingine amesema, ni kuongeza matumizi ya mifumo ya kifedha na kupunguza utegemezi wa pesa taslimu na gharama za huduma za kifedha.
Mshihiri amesema kuwa,mifumo ya malipo kidijitali inarahisisha na kuharakisha shughuli za malipo, hivyo wananchi wanaweza kufanya miamala popote walipo, kununua bidhaa, kulipia bili na nyinginezo.

Pia amesema,malipo ya kidijitali hutoa usalama mkubwa zaidi kuliko malipo ya fedha taslimu, kwani inakuwa vigumu kwa wahalifu kuiba au kuingilia malipo hayo.

Aidha,amesema kwa kutumia mifumo ya malipo kidijitali, wananchi wanapunguza gharama zinazohusiana na kubeba fedha taslimu, kama vile malipo ya huduma za benki au gharama za usafiri kwenda kwa taasisi za kifedha.

Vilevile, mifumo hiyo inaruhusu watu wengi hasa wale walioko maeneo ya mbali kama vijijini kupata huduma za kifedha kwa urahisi kupitia simu za mkononi au mtandao.

Mbali na kuwezesha kurahisisha wananchi kupata mikopo kwa haraka, pia mifumo hiyo inawezesha ufuatiliaji wa malipo kwa urahisi hivyo kuboresha huduma bila udanganyifu nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news