DAR-Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha, Bw. Jumanne Juma (28) aliyekuwa mkazi wa mtaa wa Kimara B, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam aliyeuawa kwa kuchomwa na mafuta ya petroli na watu aliokuwa akiwafanyia kazi za nyumbani kwa madai ya kuwaibia kiasi cha shilingi 200,000.
Taarifa kutoka Jeshi la Polisi na vyombo vya habari zinaeleza kuwa watu waliomuua Bw.Jumanne walimfuata nyumbani kwake majira ya saa 4 usiku kumtaka waondoke naye wakamlipe malipo yake pamoja na kumpatia kazi nyingine.
Hata hivyo, baada ya kuondoka naye walimpeleka mahali, wakanunua mafuta ya petroli na kumchoma moto.
Katika ufuatiliaji wake THBUB imebaini yafuatayo:
i. Baadhi ya wananchi bado hawaheshimu Katiba ya Nchi kama inavyoelekeza katika Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na sheria za Nchi na hivyo kujichukulia sheria mikononi.
ii. Vitendo vya mauaji vinavyotokea hivi karibuni vimeambatana na ukatili dhidi ya ubinaadamu na
iii. Kuna viashiria vya wananchi kutokuwa na imani na vyombo vya usimamizi wa haki.
Kutokana na tukio hilo ambalo limesababisha kifo cha Bw. Jumanne Juma, THBUB inapenda kutamka kuwa kitendo hicho ni :
i. Ukiukwaji wa haki ya kuishi kama ilivyotamkwa katika Ibara ya 14 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na hivyo inalaani vikali vitendo hivyo; na
ii. Ukatili dhidi ya binaadamu ambao ni kinyume na Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
THBUB inatambua jitihada za zilizofanywa na Jeshi la Polisi kwa kuwakamata watuhumiwa. Pamoja na hayo, THBUB inapendekeza yafuatayo:
1. Jeshi la Polisi Tanzania
■ Liendelee kuchukua hatua mahsusi kuimarisha ulinzi katika maeneo ya wananchi na kuwezesha kuapata taarifa za mapema kuhusu kuwepo viashiria vya uvunjifu wa sheria ikiwa ni pamoja na mauaji na vitendo vya ukatili.
■Liimarishe ulinzi shirikishi kupitia vituo vya Polisi kata kwa kuongeza idadi ya vituo na idadi ya askari ili kuongeza ufanisi.
2. Serikali za Mitaa
■ Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ngazi zote ziwe na mipango madhubuti ya kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.
3. Viongozi wa Dini
■Waongeze nguvu katika utoaji wa elimu ya dini na maadili na kukemea uovu unaotokea nchini.
4. Wananchi
■Wajenge utamaduni wa kuheshimu sheria za nchi, haki za binaadamu, kufuata namna bora ya kupata suluhu ya migogoro na kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi.
■Washirikiane na vyombo vya dola kufichua maovu kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili kuzuia matukio kama hayokutokea.
5. Asasi za Kiraia na vyombo vya Habari
■Kuendelea kutoa taarifa za matukio ya uhalifu kwa wakati na kushiriki kwa ukamilifu katika kutoa elimu kwa umma kuhusu taratibu zilizopo za namna ya kushuhulikia masuala mbalimbali ya kijamiikupitia sheria na hivyo kulinda haki za binaadamu na utu wa mtu.
THBUB inatoa pole kwa ndugu, jamaa na wanafamilia waliopoteza mpendwa wao katika tukio hili na inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika jitihada za kukomesha na kulinda haki za binaadamu na misingi ya Utawala Bora
Jukumu la ulinzi na utetezi wa haki za binaadamu ni letu sote!
Imetolewa na:
Mathew P.M. Mwaimu (Jaji Mstaafu)
MWENYEKITI
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA.