Tunanunua dhahabu ya Tanzania tu-BoT

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia Mpango wa Ununuzi wa Dhahabu nchini imefanikiwa kununua tani zaidi ya mbili za dhahabu ndani ya miezi mitano, lengo ni kuongeza akiba ya dhahabu,kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kuinua soko la madini nchini.
Mpango huo unatoa fursa kwa wauzaji wa dhahabu nchini kuuza dhahabu zao moja kwa moja kwa BoT kwa bei ya ushindani ya Soko la Kimataifa.

Mchambuzi wa Masoko ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Dunga Nginila ameyasema hayo leo Februari 25,2025 mkoani Mtwara katika semina kwa waandishi wa habari za uchumi,biashara na masoko ya fedha inayoratibiwa na BoT.

Akiwasilisha mada ya umuhimu wa akiba ya dhahabu kama sehemu ya hifadhi ya taifa ya fedha za kigeni,Nginila amesema kuwa,lengo la Benki Kuu kwa mwaka ni kununua tani sita za dhahabu kutoka nchini.

“Dhahabu ina faida kubwa, hususani nchi kama yetu ambayo tumejaliwa kuwa na dhahabu nyingi, kwa hiyo kikubwa ni kwamba tunaongeza akiba ya fedha za kigeni za nchi hususani dhahabu fedha, tunapoinunua na tunapoifikisha katika custody zetu inahesabika kama fedha za kigeni za nchi.

“Kwa hiyo,mpaka sasa tume-accumulate tani zaidi ya mbili mpaka sasa,na lengo la Benki Kuu ni kununua tani sita kwa mwaka, na tunatarajia kufikia hilo lengo kabla ya mwaka wa fedha huu kukamilika.

“Kitu cha muhimu na msingi ni kwamba tunanunua dhahabu ya Tanzania tu, si dhahabu ya nchi nyingine,kwa hiyo huu mpango wa BoT, tunanunua dhahabu kila siku kwa sababu tuna target ya mwaka.”

Kupitia mpango huo ambao ulianza Oktoba 7,2024 wauzaji wa dhahabu wanapata punguzo la ada na uhakika wa malipo ya haraka wakiuza asilimia 20 ya dhahabu zao Benki Kuu kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini (Sura ya 123).

Aidha, bei ambayo huwa inatumika ni ile ya dhahabu duniani kama inavyotolewa na Tume ya Madini ambapo huwa inababilika kila siku.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news