ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Alhaji Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza waumini wa Dini ya Kiislamu kuweka mkazo wa kuwasaidia masikini,wajane na yatima ili kuwapa unafuu wa maisha wakati wa kufunga Ramadhani.
Alhaj Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipotoa salamu kwa waumini wa Masjid Hamieni Muyuni C Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kujumuika katika Dua Maalum ya kuwaombea viongozi wakuu wa nchi na Sala ya Ijumaa.
Aidha,Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa,jamii ina wajibu mkubwa wa kuyasaidia makundi hayo maalum kwani ni thawabu kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu ili nao wafunge kwa utulivu.
Halikadhalika Alhaj Dkt.Mwinyi amewakumbusha wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa za vyakula wakati wa Ramadhani ili wananchi wamudu kununua bidhaa hizo.
Akizungumzia suala la amani,Alhaj Dkt.Mwinyi amewasihi wanasiasa,viongozi wa dini na waumini kwa ujumla kulichukua suala la amani kuwa ajenda namba moja katika hutuba zao ili nchi iendelee kuwa na amani.
Akizungumzia suala la malezi,Alhaj Dkt. Mwinyi amehimiza kwa vijana kuelimishwa elimu ya dini na kutoa rai kwa Miskiti na Madrasa kutekeleza wajibu huo.