NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi popote pale walipo nchini kuhakikisha wanapokopa mikopo katika taasisi mbalimbali wahakikishe inatumika kwa shughuli za maendeleo na si starehe.
Afisa Mkuu Mwandamizi, Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Deogratias Mnyamani ametoa rai hiyo leo Februari 17,2025 katika maeneo ya Mabibo Mwisho jijini Dar es Salaam.

Kampeni hiyo iliyoanza Januari 30, 2025 imejikita katika kuelimisha umma kuhusu ukopaji salama unaozingatia kutumia wakopeshaji wenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania.
Aidha,kupitia masharti na vigezo vya mkopo kabla ya kusaini na kupokea mkopo pamoja na kukopa kwa malengo ya kiuchumi na maendeleo.
"Lakini tumeona pia kwamba, Mtanzania anapaswa kukumbushwa jambo la muhimu kwamba tunapokopa, tukope kwa maendeleo.
"Tusikope tu kwa sababu tumepata shida, chukua mkopo kwa sababu unataka kupeleka kwenye shughuli ya uzalishaji,kwenye shughuli ambayo itakusaidia kurejesha marejesho.
"Tumekutana na changamoto nyingi kwamba Watanzania wengi wanakopa, lakini wanazipeleka zile pesa kwenye mambo ambayo hayatawasaidia kupata kipato cha kurejesha marejesho.
"Kwa mfano, dada zetu, Shangazi zetu na mama zetu wanachukua mikopo wanaenda kufanyia sherehe, wanaenda kutunzana na vitu kama hivyo.
"Sasa, yale matukio hayawasaidii kuweza kurejesha marejesho, kwa hiyo kampeni yetu inamlenga mlaji, kumzindua, kwani Watanzania wengi wameangamia kwa sababu walikuwa usingizini, tumelijua hilo kwa hiyo tumelenga kumzindua Mtanzania ili ajue wajibu wake, ajue haki zake, ajue wapi pa kujitetea, ajue wapi pa kupeleka malalamiko na pia awe na nidhamu ya mikopo anayochukua."
Bw.Mnyamani amesema, Benki Kuu inafanya kampeni hiyo kwa sababu, "tunaona licha ya kuwepo sheria nzuri ya huduma ndogo za fedha, kanuni nzuri, miongozo mizuri na sera nzuri bado Watanzania wanaendelea kuumia kwenye suala la mikopo.
"Tumefanya utafiti na kugundua kwamba kinachowafanya kuendelea kuumia ni kwa sababu ya kukosa uelewa."
Pia, amesema wananchi wanakosa uelewa wa kujua ni vitu gani ni vya muhimu na haki zao ni zipi wakati wanakwenda kwenye mikopo.
Jambo lingine amesema, ni wananchi kutotambua wajibu wao wakati wa kwenda kuchukua mikopo.
"Kwa hiyo, wanapokutana na watoa huduma ambao siyo waaminifu wanawaumiza. Ninyi ni mashaidi kwamba, Watanzania wamenyanyaswa.
"Wamedhulumiwa, wamepata hasara nyingi kwenye suala hili la mikopo mpaka majina mengi yametokea kutokana na suala hili.Kwa hiyo, Benki Kuu ilipoona hiyo changamoto ikaona iitatue na utatuzi wake ni kutoa elimu kwa umma.
"Na moja ya kampeni ambayo tunatumia ni hii ya kutumia matangazo ambayo yanapita mtaa kwa mtaa jijini Dar es Salaam, mpaka sasa hivi tunavyoongea tumeshamaliza Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni, Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam."
Amesema kwa sasa wanaendelea na vitongoji vya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni na Ubungo ambapo kampeni hiyo inapita mtaa kwa mtaa,vitongoji kwa vitongoji na kuna maeneo imevuka hadi mipaka ya Jiji.
"Lengo ni kumuelimisha Mtanzania, unapokwenda kukopa awe na tija muhimu anazozizingatia. Kampeni hii, tumekuja nayo kwa sababu kama mnavyoona Watanzania wengi tunawakuta katika shughuli zao za kawaida, pale walipo hawana TV, hawana redio, hawana gazeti.
"Pale walipo hawana muda wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii kila mtu ambaye yupo katika biashara yake pale sokoni.Kwa hiyo,tunamtembelea kila Mtanzania tunaongea naye."
Amesema,kupitia kampeni hiyo kwa siku wana uwezo wa kuwafikia Watanzania 3000 kupitia mtaa kwa mtaa na vitongoji kwa vitongoji.
Vilevile, Mnyamani amesema, wataalum wamekuwa wakipita kijiwe kwa kijiwe na kufanya mazungumzo na wananchi huku wakitoa maoni yao.
"Siyo tu kwamba wanatoa elimu, wanapokea maoni na kupata mrejesho kutoka kwao kwa sababu pia sisi tunafanya utafiti kupitia kampeni yetu ili kujua ni changamoto gani zinawakumba wananchi na nini kinawapekekea kukopa."
Amesema, kampeni hiyo imejikita katika maeneo muhimu ikiwemo kumwelimisha Mtanzania kuhakikisha anafanya kila linalowezekana kukopa katika taasisi ambazo zimepewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
"Tunasema hivi kwa sababu,atakapokutana na madhila mbele ya safari kwa sababu yule ni mtu ambaye tumempa sisi leseni, tunajua namna ya kumrudisha kwenye mstari na yule mteja atapata haki yake."
Jambo lingine amesema, wamebaini Watanzania wengi hawasomi vigezo na masharti wanapochukua mikopo.
"Wanapochukua mikopo wanachukua mikopo tu kwa sababu wana shida fulani,hawaangalii mikopo hiyo ina mikataba gani, vigezo ni vipi na masharti ni yapi."
Amesema, kampeni hiyo inasisitiza Mtanzania ajiridhidhe kwamba amesoma, ameelewa na ametafakari vizuri vigezo na masharti ambayo vipo kwenye mikataba ya mikopo.
"Lakini, kama haitoshi tunamwambia Mtanzania achukue nakala,asiache kuchukua nakala ya mkataba ya ule mkopo anaouingia. Watanzania wengi wanaokuja pale kwetu kulalamika, hawana nakala ya Mkataba, kwa hiyo tunashindwa namna ya kuwasaidia."
Amesisitiza kuwa, kila mmoja achukue nakala ya mkataba ambao wameingia kwani tayari walishawaambia watoa huduma.
Pia, amesema kampeni hiyo inawakumbusha Watanzania kuhusu wajibu wao wa kurejesha mikopo baada ya kukopa.
"Kwa hiyo tunamkumbusha Mtanzania anapokopa arejeshe marejesho yake kwa wakati."
Vilevile, ameeleza kuwa kampeni hiyo inawakumbusha Watanzania kuwa, wanapokutana na malalamiko huo sio mwisho wa maisha.
Kwani, wanaweza kufika Benki Kuu ambapo kuna dawati la kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wateja ambapo utaratibu unapaswa kuanzia kwanza kwa mtoa huduma.
"Ikiwa hatakupa majibu ambayo yanajitosheleza, sasa kuna dawati liko rasmi Benki Kuu kwa ajili ya kupokea malalamiko ya wateja."