DAR-Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mheshimiwa Lord Collins amevutiwa na mpango wa nchi ya Tanzania kuandaa mkakati maalum wa uongezaji thamani madini nchini Tanzania na kuahidi kwamba Uingereza itatoa ushirikiano katika kusaidia eneo la uongezaji thamani madini hayo ndani ya nchi.
Hayo yamesemwa leo wakati wa kikao kati ya Mheshimiwa Lord Collins na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
“Tanzania na Uingereza zina ushirikiano wa muda mrefu katika maeneo mengi ya kiuchumi ikiwemo sekta ya Madini.
"Nimevutiwa na mkakati wa Tanzania wa kuongeza thamani ndani ya nchi, mkakati ambao Uingereza tunauunga mkono na tupo tayari kuwezesha utekelezaji wake kupitia Mradi wa Manufacturing Africa ambapo ya pauni 2.1 bilioni zimetengwa kusaidia nchi 6 za Afrika,ikiwemo Tanzania,kutengeneza bidhaa za kati na za mwisho kupitia madini,“alisema Lord Collins.


Serikali imetenga eneo maalum la ujenzi wa viwanda vyakuongeza thamani wilayani Kahama,Mkoani Shinyanga kwa lengo la kuvutia uwekezaji katika eneo hili.
“Mradi wa Manufacturing Africa utasaidia kufanikisha azma ya Tanzania kwa kuwezesha uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata,kusafisha na kutengeneza bidhaa zitokanazo na madini,“amesema Mavunde.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza,Mheshimiwa Mbelwa Kairuki na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania,Mheshimiwa Marianne Young.