ZANZIBAR-Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe.Tabia Maulid Mwita amesema lengo kuu la ujenzi wa Nyumba ya Sanaa ni kuibua, kuvikuza na kuvitangaza vipaji vya sanaa kwa vijana.
Ameyasema hayo huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi B wakati alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwererkwe, Mhe. Ameir Abdallah Ameir.
Aidha,amesema lengo jingine ni kuimarisha, kuhifadhi na kuendeleza Utamaduni na Sanaa ya Zanzibar.
Sambamba na hayo Waziri Tabia amesema, vijana watapata fursa ya kujifunza ujuzi wa sanaa mbalimbali, kuonesha kazi za utamaduni ikiwa ni hatua moja wapo ya kurithisha amali za sanaa na utamaduni wa Zanzibar.
Hata hivyo,amesema matarajio ya mradi ni kuona vijana wanapata ujuzi wa kazi za Sanaa na Utamaduni, vijana wanajishughulisha na kazi za amali zitakazowapatia kipato, kuibua vipaji na kuviendeleza.
Mbali na hayo ameitaka jamii kufuata maadili na kuepukana na vitendo vya udhalilishaji na utumiaji wa dawa za kulevya.