DODOMA-Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Mhe. Dkt. Festo Dugange, amesema kuwa ukomo wa umri wa vijana wanaostahili kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri umeongezwa kutoka miaka 35 hadi 45.
Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo bungeni jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Bunda, Mhe. Boniphace Mwita Getere aliyetaka kujua ni lini Serikali itatenga dirisha maalum la mikopo kwa wanaume waliovuka umri wa vijana.
Akijibu swali hilo, Dkt. Dugange ameeleza kuwa mikopo hiyo ya asilimia 10 hutolewa kwa makundi maalum ya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kwa masharti nafuu bila riba, kwa kuwa makundi hayo yana changamoto ya kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha kutokana na ukosefu wa dhamana na uwezo wa kumudu riba kubwa.
"Ukomo wa umri wa vijana wanaostahili kupata mikopo sasa umeongezwa kutoka miaka 35 hadi 45," amesema Dkt. Dugange.
Katika swali la nyongeza, Mhe. Getere amehoji ni lini Serikali itatoa mwongozo rasmi kwa Halmashauri ili wananchi wa vijijini wapate ufahamu kuhusu mabadiliko hayo.
Dkt. Dugange amefafanua kuwa baada ya kukamilika kwa kanuni za mikopo ya asilimia 10 za mwaka 2024, tayari miongozo imeshatolewa na kusambazwa kwa Halmashauri zote 184.
Amesisitiza kuwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 45 sasa wanastahili mikopo hiyo, huku akitoa wito kwa wakurugenzi wa Halmashauri kote nchini kuhakikisha elimu inatolewa kwa wananchi ili kuongeza idadi ya wanufaika.