PWANI-Baadhi ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Pwani wamepatiwa mafunzo kuhusu uandishi wa habari zinazohusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM). Mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Anjita kwa kushirikiana na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Pwani na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, yalifanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa mjini Kibaha.
Yalifadhiliwa na Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Tanzania (TECDEN).
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Zablon Bugingo, alishukuru taasisi ya Anjita kwa kutoa mafunzo hayo muhimu kwa waandishi wa habari. Alieleza kuwa mradi wa MMMAM unatekelezwa na serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, kwa kushirikiana na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Afisa Programu na Mafunzo kutoka UTPC, Victor Maleko, ambaye pia alikuwa mkufunzi wa mafunzo hayo, alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari katika kuleta mabadiliko chanya kwenye masuala ya malezi na makuzi ya watoto.
Alibainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa katika uandishi wa habari kuhusu MMMAM, ambayo ni programu mama ya kitaifa inayotekelezwa kwa ushirikiano wa serikali na taasisi mbalimbali, ikiwemo UTPC.
Akifunga mafunzo hayo, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha, Elia Kabora, alieleza kuwa programu ya MMMAM inalenga kukuza watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 8 katika nyanja za kimwili, kiakili, lugha, kijamii, kitamaduni, kihisia, na kimaadili.
Programu ya MMMAM ni juhudi ya pamoja kati ya serikali na wadau mbalimbali, ikiwemo Children in Crossfire (CiC), TECDEN, na UTPC, yenye lengo la kuboresha maisha ya watoto katika nyanja za afya bora, lishe, ujifunzaji wa awali, ulinzi na usalama, pamoja na malezi yenye mwitikio.