ZANZIBAR-Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ndugu Abeida Rashid Abdallah amesema, wizara hiyo inatarajia kupokea ujumbe mkubwa wa wadau wa maendeleo katika masuala ya jinsia.
Ni kutoka katika Mashirika ya Kimataifa ambayo wawakilishi wake wapo hapa nchini, ikiwemo UN Women, UNFPA, UNICEF, European Union na wawakilishi wa Ofisi za Kibalozi.
Ameyasema hayo leo Februari 10,2025 jijini Zanzibar katika mkutano na wanahabari kwa ajili ya kutoa taarifa ya ziara ya wadau wa maendeleo katika masuala ya jinsia (Development Partners Group Gender Equality DPG-GE).

"Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatarajia kupokea ujumbe mkubwa wa Wadau wa Maendeleo katika masuala ya jinsia kutoka katika Mashirika ya Kimataifa ambayo wawakilishi wake wapo hapa nchini, ikiwemo UN Women, UNFPA, UNICEF, European Union na Wawakilishi wa Ofisi za Kibalozi."
Pia, amesema wizara hiyo inatarajia kupokea viongozi na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
"Ambayo ndio wizara pacha tunayofanya nayo kazi kwa mashirikiano makubwa. Kwa ufupi wizara inategemea kupokea ujumbe wa watu 60.
"Shukrani za dhati zimwendee Mhe. Dkt Dorothy Gwajima Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Katibu Mkuu wake Dkt. John Jingu kwa mashirikiano makubwa wanayotupa katika utekelezaji wa shughuli zetu."
Amesema,lengo la ziara hiyo ni kutembelea baadhi ya maeneo ya utekelezaji wa program za kijinsia chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).
Kabla ya kwenda kutembelea programu hizo, Wageni hao watakutana na Waziri dhamana wa Wizara hii, Mheshimiwa Riziki Pembe Juma.
"Hii ni ziara ya siku tatu katika mikoa yote mitatu ya Unguja. Miongoni mwa maeneo yatakayotembelewa ni pamoja na Dawati la Jinsia lililopo Makao Makuu ya Polisi Ziwani, Kituo cha Mkono kwa mkono kilichopo katika Hospitali ya Kivunge, Umoja wa waanika dagaa wanawake uliopo Mangapwani, na Chuo cha Barefoot College kiliopo Kinyasini."
Amesema,kwa Mkoa wa Kusini Unguja watatembelea wakulima wa mwani Muungoni na kikundi cha wanawake kinachojulikana kwa jina la TUFAHAMIANE kilichoko Kizimkazi.