WASHINGTON DC-Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) limevunja ukimya kuhusu mustakabali wa wafanyakazi wake.
Ni baada ya hatua mpya iliyochukuliwa na Rais Donald Trump ya kusitisha ufadhili wa shirika hilo ambalo limekuwa likihudumia mamilioni ya watu duniani.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj8rFeZwMkbfU3ke-JWRQov_dIFceq1jUfQa_Ez0zxPLNEEglPfpd-RrHFFztbNcjNOfoWPr_4H5osDNoKSL2BMiz0LhSiFjHUzvHPIRXyj4jbVAUU5RkF6wqEB5hK9R4TSscGuvwkzwkbX5Z5A-QTnjY2vYxknaH-GstwOMNaqVvAuIbTA_9xOJeMwo0e6/s16000/1001171301.jpg)
Kwa mujibu wa taarifa ya USAID kuanzia Ijumaa, Februari 7, 2025 majira ya saa tano na dakika 59 usiku (kwa saa za Marekani) wafanyakazi wake wa moja kwa moja kote duniani watawekwa kwenye likizo ya kiutawala, isipokuwa wale waliochaguliwa kushughulikia majukumu muhimu.
"Kuanzia Ijumaa, Februari 7, 2025, saa 5:59 usiku (EST), wafanyakazi wote wa USAID walioajiriwa moja kwa moja watawekwa kwenye likizo ya kiutawala kimataifa, isipokuwa wale walioteuliwa kwa kazi muhimu," inasema taarifa ya USAID.
Aidha,kwa mujibu wa shirika hilo, wafanyakazi waliotarajiwa kuendelea na kazi watajulishwa kufikia Februari 6, 2025.
Kwa wafanyakazi wa USAID walioko nje ya Marekani, shirika hilo limetangaza kuwa, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani linaandaa mpango wa kuwarejesha nyumbani ndani ya siku 30.
Wakati huo huo,Marekani imeufahamisha rasmi Umoja wa Mataifa kwamba imesitisha ufadhili wake kwa kikosi kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambacho kilikuwa na jukumu la kupambana na magenge yanayojaribu kudhibiti mji mkuu wa Haiti, Umoja wa Mataifa ulisema Jumanne.
Marekani imekuwa mfadhili mkubwa wa kikosi hicho kinachoongozwa na polisi wa Kenya, ambacho kilianza shughuli zake mwaka jana na kinakabiliwa na ukosefu wa fedha na wafanyakazi.
Kusitishwa kwa ufadhili huo kutakuwa na athari za moja kwa moja kwa kikosi hicho, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema.
Hatua hiyo inajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutoa amri ya kuzuia misaada ya kigeni, na kusababisha maelfu ya wafanyakazi na wanakandarasi wa USAID kuachishwa kazi na program nyingi za idara hiyo kusitishwa ulimwenguni kote.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio aliruhusu program za kuokoa maisha ziendelee, lakini bado kuna mkanganyiko kuhusu kipi kinaruhusiwa kutolewa katika amri ya kiutendaji ya rais na hofu ya kukosa misaada ya Marekani kabisa, inakwamisha utoaji wa misaada na kazi ya maendeleo duniani kote.
Marekani ilikuwa imeahidi kutoa dola milioni 15 kwa mfuko wa Umoja wa Mataifa unaosaidia kufadhili kikosi cha Kimataifa nchini Haiti, Dujarric alisema.
"Dola milioni 1.7 zimekwisha tumiwa, dola milioni 13.3 sasa zimezuiliwa,” Dujarric aliongeza.
Mfuko huo wa Umoja wa Mataifa unasalia na chini ya dola milioni kwa jumla ya dola milioni 600 zinazohitajika kila mwaka kwa kikosi hicho cha kimataifa.
Maafisa wanaoongoza kikosi cha Kenya hawakutarajia usitishwaji wa ufadhili huo. Msemaji wa kikosi hicho Jack Mbaka hakutoa maelezo ya mara moja kwa shirika la habari la AP. (NA/VOA).