MARA-Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi tarehe 17 Februari, 2025 ameitembelea kambi ya wagonjwa wa kuharisha na kutapika katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na kuwaagiza wakuu wa Wilaya za Musoma na Rorya pamoja na wataalamu wa Halmashauri kutoka ofisini na kushughulikia chanzo cha ugonjwa huo.
Mhe. Mtambi ametoa maagizo hayo katika Zahanati ya Bwai ambayo kwa sasa inatumika kama Kituo cha Halmashauri ya Musoma kwa ajili ya kutibu wagonjwa wa kuharisha na kutapika katika eneo hilo na kujionea hali halisi ya kituo hicho na kuzungumza na viongozi, wataalamu na wananchi waliokuwepo eneo hilo.

“Ninawataka Wakuu wa Wilaya na Wataalamu wa Halmashauri za Wilaya ya Musoma na Rorya kutoka ofisini na kufanya kampeni maalum ya ujenzi wa vyoo katika maeneo ambayo yamekumbwa na tatizo hilo na kushughulikia chongamoto zozote zinazoweza kuendeleza changamoto hizi katika maeneo yao,” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amezitaka Wilaya hizo kuanzisha operesheni maalum ya kukagua vyoo bora na salama na matumizi ya vyoo hivyo na hususan maeneo yenye mikusanyiko kama vile kambi za wavuvi, masoko na majengo ya huduma mbalimbali kuhakikisha yana vyoo vinavyotumiwa na wananchi.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa eneo hilo na Mkoa wa Mara kwa ujumla kubadilisha namna wanavyoishi maisha yao na kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya wataalamu wa afya ili kujilinda na kuwataka katika hili wasisubiri kusukumwa.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa Halmashauri za Wilaya ya Rorya na Musoma zina wagonjwa wa kutapika na kuharisha na kuwataka viongozi kuchukua hatua za haraka na maksudi kukabiliana na chanzo cha tatizo hilo ambalo ni matumizi ya vyoo safi na salama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Dkt. Joseph Fwoma amesema tangu tatizo hilo lilipoanza Januari 23, 2025 Halmashauri hiyo imepata jumla ya wagonjwa 63 na kati yao mmoja amefariki dunia na wengine kuruhusiwa baada ya kupona na wagonjwa tisa tu ndio wanaendelea na matibabu katika kituo hicho.
Dkt. Fwoma amesema tatizo hilo linatokana na kuwepo kwa mwalo mkubwa wa wavuvi katika eneo hilo pamoja na kisiwa kilichopo jirani ambacho kinachokaliwa na wavuvi jirani na Zahanati ya Bwai na ndio sababu ya kuchagua zahanati hiyo kama kituo cha halmashauri cha kuwahudumia wagonjwa hao.
Bwana Fwoma amesema jitihada mbalimbali zimefanyika na Halmashauri pamoja na Mkoa ikiwa ni pamoja na kuwahamishia wataalamu zaidi katika kituo hicho, kuweka dawa za kutosha, kusambaza dawa za kutibu maji, kuwahamishia wagonjwa wa kawaida katika majengo mapya ya Kituo cha Afya Bwai kilichopo jirani na eneo hilo na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Akizungumza katika kituo hicho, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amesema kama Wilaya wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuwahamasisha wananchi kujenga na kutumia vyoo bora na hususan katika vijiji vilivyoko kando kando ya ziwa.
“Tayari jitihada mbalimbali zimeshafanyika ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wananchi na kuwaagiza RUWASA Wilaya ya Musoma kukamilisha kwa haraka mradi wa maji unaotekelezwa katika Kata ya Busambara ili wananchi wa eneo hili wapate maji safi na salama,” amesema Mhe. Chikoka.
Mhe. Chikoka ameahidi kuongeza nguvu kwa kufanya operesheni maalum ya kutoa elimu pamoja na kuhamasisha ujenzi na matumizi ya vyoo, kuchemsha maji ya kunywa na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya katika eneo hilo. 

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bwai Dkt. Justus Francis Haule amesema hadi wakati Mkuu wa Mkoa anatembelea, kituo hicho kilikuwa na wagonjwa tisa ambapo kati yao wagonjwa saba ni wanaume huku wawili wakiwa ni wanawake.
Dkt. Haule amesema kwa sasa kituo hicho kina dawa zote muhimu za kukabiliana na tatizo hilo na tayari Halmashauri imeagiza dawa nyingine kama ugonjwa wa kuharisha na kutapika utaendelea katika eneo hilo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mtambi aliambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama wa Wilaya ya Musoma, baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkurugenzi na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, viongozi wa vijiji na Kata wa eneo hilo.