DAR-Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dk Peter Kisenge amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za matibabu katika taasisi hiyo.
Wanachama wa Jumuia ya Moyo ni Uhai ambao ni wagonjwa waliofanyiwa na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Jumuia hiyo uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI. Jumuia hiyo ina wanachama zaidi ya 300 waliofanyiwa upasuaji wako zaidi ya 140 na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wako zaidi ya 160.
Amesema maboresho yaliyofanyika kwenye taasisi hiyo si tu yamekuwa yakiwasaidia Watanzania bali hata raia wa kigeni wanakuja nchini kufuata matibabu ya moyo.
Dkt. Kisenge ameyasema hayo katika mkutano wa kwanza wa mwaka wa wa Jumuiya ya Moyo ni Uhai ambao ni wagonjwa waliofanyiwa upasuaji na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam.
Jumuiya hiyo yenye wanachama zaidi ya 300 kati yao zaidi ya 140 wamefanyiwa upasuaji wa moyo na zaidi ya 160 wanasubiri kupata huduma hiyo.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Bashir Nyangasa akitoa elimu ya lishe na matumizi sahihi ya dawa za moyo kwa wanachama wa Jumuiya ya Moyo ni Uhai ambao ni wagonjwa waliofanyiwa na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo wakati wa mkutano wao mkuu wa kwanza uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Dkt. Nyangasa ni Ramadhani Kampira ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuia hiyo na mchezaji wa zamani wa timu ya Yanga.
“Niwashukuru viongozi wetu katika sekta ya afya kwa namna wanavyotuongoza kuwahudumia wananchi,”alisema Dkt.Kisenge.
Mbali na hayo Dkt. Kisenge alisema madaktari wa JKCI watatumia Jumuiya ya wagonjwa wa moyo kutoa elimu ya magonjwa ya moyo ambayo yanachangia vifo vingi duniani na kwa kiasi kikubwa maradhi hayo yanazuilika.
Kuhusu gharama za matibabu ya moyo alizosema ni kubwa, amesisitiza ukubwa wa gharama hizo si kwenye hospitali hiyo pekee bali ni duniani kote.
“Nafahamu mmeeleza changamoto nyingi ambazo zipo, gharama za matibabu ya moyo ni kubwa sana na si kwetu tu, ukifanyiwa upasuaji ni karibu Sh15 milioni, jumuiya hii itakaa pamoja na sisi tuangalie ni jinsi gani ya kupunguza ili watu wengi wapate hii huduma,”alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wanachama wa Jumuia ya Moyo ni Uhai ambao ni wagonjwa waliofanyiwa na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo wakati wa mkutano wao mkuu wa kwanza uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Jumuia hiyo ina wanachama zaidi ya 300 waliofanyiwa upasuaji wako zaidi ya 140 na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wako zaidi ya 160.
Awali Mwenyekiti wa Jumuiya ya Moyo ni Uhai Editha Ngoitanile alisema alifanyiwa upasuaji wa moyo mwaka 1999 nchini India na maisha yake yamekuwa yakiendelea vyema.
Alisema taasisi hiyo inajumuisha watu waliofanyiwa upasuaji wa moyo nchini Tanzania na India na walianzisha jukwaa hilo kwa lengo la kueleza changamoto zao kwa urahisi.
“Sisi watu wa moyo tusiishi kinyonge tumeanzisha chama watu wasikae kinyonge, mkurugenzi wa JKCI ametupa fursa nyingi na sisi tumeambiwa tunaweza kupata bima ya afya ya vikundi na kupewa kadi za utambulisho,”alisema.
Naye mchezaji wa zamani wa Yanga Ramadhani Kampira ameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya.
“Nilivyokuja hospitali niliambiwa nina ugonjwa wa moyo tangu miaka 10 iliyopita, nilikuwa naanguka mazoezini kuna kijana akanishauri nikaangalie moyo nilivyofanya uchunguzi nikaambiwa mishipa mitatu ya damu ya moyo imeziba hivyo nikahitajika kufanyiwa upasuaji,”alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akitoa cheti cha shukrani kwa Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Bashir Nyangasa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha Taasisi hiyo Anna Nkinda kilichotolewa na Jumuia ya Moyo ni Uhai kwa kutambua mchango wa JKCI wa kuwapatia huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo.
Alisema wakati huo hali yake ya afya ilikuwa ngumu hata kutembea hatua tatu au kukimbia kutokana na maumivu makali ya kifua alikuwa hawezi lakini baada ya kufanyiwa upasuaji amepona na anaendelea vizuri.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Bashir Nyangasa aliwakumbusha wanachama wa Jumuia hiyo kufuata maelekezo ya wataalamu wanayopewa katika utumiaji wa dawa pamoja na ulaji wa vyakula bora.