Watendaji Sekta ya Ardhi watakiwa kuzingatia uadilifu katika utoaji huduma za ardhi nchini

MOROGORO-Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Geofrey Pinda amesema, Serikali inaendelea kusimamia ufuatiliaji wa tathimini katika utekelezaji wa majukumu ya ardhi na uadilifu katika utoaji wa huduma za ardhi nchini.
Mhe.Pinda ameeleza hayo leo mkoani Morogoro wakati akifungua mkutano wa sekta ya ardhi mkoani humo.

"Hatua muhimu za kinidhamu na ufuatiliaji zilizochukuliwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi na uwazi katika utoaji wa huduma,"amesema.
Naibu Waziri Pinda ameeleza kuwa Wizara kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali itaendelea na utaratibu wa kutatua migogoro katika mikoa yenye changamoto ya sekta ya ardhi ukiwemo mkoa wa Morogoro.

Katika hatua nyingine Mhe.Pinda amewakumbusha watumishi wa Wizara hiyo kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii kuwahudumia wananchi vizuri kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
"Watumishi wenzangu tukumbuke uadilifu katika kazi, kazi ni hazina kwa mtumishi, wengine nikiwatazama hapa wengi ni vijana. h

"Hivyo, bado mna fursa kubwa ya kiutumishi mkifanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu," amesema Naibu Waziri Pinda.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Morogoro Idrisa Kahyera amesema kuwa kuanzia Februari 26 hadi Machi 1 mwaka huu kutafanyika Kliniki ya Ardhi katika Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuwahudumia wananchi wa mkoa huo.

"Katika Kiliniki hiyo tutatoa huduma mbalimbali zikiwemo uandaaji na utoaji hati kwa muda mfupi, kutoa vibali vya ujenzi, kukadiriwa Kodi za ardhi, kusikilizwa kwa mashauri ya Ardhi na wenyeviti wa Baraza la Ardhi," ameeleza.
Mkutano wa Sekta ya Ardhi mkoani humo umejumuisha Watumishi wa Ardhi kutoka Halmashauri zote 9 za Mkoa wa Morogoro, Mabaraza ya Ardhi,Shirika la Nyumba,Chuo cha Ardhi Morogoro na tume ya Mipango Bora ya Ardhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news