Watumishi TFRA watakiwa kufanya kazi kwa weledi ili kukidhi matarajio ya wakulima nchini

MOROGORO-Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kujikita katika kutatua changamoto za wakulima kwa haraka na ufanisi, ili kufanikisha matarajio ya sekta ya kilimo na Serikali kwa ujumla.
Wito huo umetolewa Januari 31,2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo, wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha Mamlaka hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Morena, mkoani Morogoro.

Dkt. Diallo amesema vikao kama hivyo ni fursa muhimu kwa watumishi kutathmini mafanikio ya taasisi kwa mwaka mzima na kuweka vipaumbele vya kibajeti katika masuala ya kimkakati ili kufanikisha malengo ya TFRA na matarajio ya wakulima.
"Ni muhimu kuhakikisha kuwa tunakuwa proactive katika utendaji wetu ili kutatua changamoto za wakulima kabla hazijawa mzigo kwao. Mnaweza pia kujadiliana namna ya kuwa na vifaa vya kuweza kuhakiki taarifa wanazopewa wakulima kuhusiana na mbolea katika maeneo mnayosimamia, ili kuimarisha huduma na kuleta tija katika sekta ya mbolea," amesema Dkt. Diallo.

Aidha, amewataka wajumbe wa baraza hilo kufanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye kikao kilichopita na kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofikiwa yanatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya sekta ya kilimo.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, alimkaribisha mgeni rasmi na kueleza kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/2025, pamoja na mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2025/2026, ambayo itawasilishwa kwenye Bodi kwa ajili ya mapitio na kuidhinishwa.
Laurent amesema kikao cha mwaka huu kilitanguliwa na mafunzo maalum kwa wajumbe wa baraza, ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kama wawakilishi wa vitengo na idara mbalimbali ndani ya TFRA.
"Kikao hiki ni jukwaa muhimu kwa kuwa kinapokea maoni yanayoakisi hali halisi ya utendaji wa taasisi, huku yakijumuisha ushiriki wa ngazi zote za watendaji. Hii ni fursa ya kujadili kwa kina jinsi ya kuimarisha utendaji wetu ili kuhakikisha huduma kwa wakulima zinaendelea kuwa bora zaidi," amesema Laurent.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutoka idara mbalimbali za TFRA, wakijadili kwa kina masuala ya utendaji na maendeleo ya taasisi hiyo kwa lengo la kuboresha sekta ya mbolea nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news