Wawili Dar wahukumiwa jela maisha kwa kusafirisha dawa za kulevya

DAR-Februari 14,2025 Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Mhe. Jaji Kisanya S.E, imewatia hatiani na kuwahukumu kifungo cha maisha jela watuhumiwa Jimmy Walter Mlaki na Stanley Salvatory Ngowi (Sultan) kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 503.63.
Hukumu hiyo ilisomwa wakati upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Hellen Masuhuli, Wakili Peter Kibatala, na Rebeca Ezekiel kwa mshtakiwa wa kwanza, huku Wakili Banana Feruzi Kalema akimtetea mshtakiwa wa pili.

Watuhumiwa walikamatwa Januari 27, 2020 katika eneo la Ubungo Kibo, Wilaya ya Ubungo, wakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Sienta, rangi ya silver, namba za usajili T 776 DSE, iliyokodiwa kama taxi.
Katika utetezi wao, washtakiwa waliomba adhabu ndogo wakidai kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na wana familia zinazowategemea.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kusikiliza hoja zote, Mahakama iliwahukumu kifungo cha maisha jela kwa mujibu wa Kifungu cha 15(1)(a) na 3(iii) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 ya 2019 pamoja na Kifungu cha 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, Sura ya 200 marejeo ya 2022.
Mahakama pia iliamuru dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 503.63 kuharibiwa kwa mujibu wa sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news