DAR-Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amemuagiza Kamishna wa Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai kushirikiana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi kufanya operesheni ya kudhibiti na kukomesha vitendo vya utapeli wa mtandaoni pamoja na wizi wa simu.
Bashungwa ametoa maagizo hayo leo, alipotembelea Maabara ya Uchunguzi wa Makosa ya Kimtandao katika Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai jijini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kila robo ya mwaka inaonesha kuwa mikoa ya Rukwa, Morogoro, Mbeya na Dar es Salaam inaongoza kwa vitendo vya utapeli wa mtandaoni, huku maeneo hayo yakiendelea kujirudia katika ripoti hizo.
“Katika kipindi cha miaka miwili, matukio ya uhalifu mtandaoni yameongezeka katika mikoa hii, ambapo Morogoro, hususan eneo la Ifakara, limeonekana kuwa kinara,” amesema Bashungwa.
Bashungwa amelitaka Jeshi la Polisi kukomesha mtandao mpana wa wahalifu wa mtandaoni, ambao hushirikiana kati ya mkoa mmoja na mwingine katika kuratibu vitendo vya wizi na utapeli.