Waziri Dkt.Nchemba azindua rasmi Moduli ya Kupokea Rufaa Kielektroniki

MWANZA-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.) amezindua rasmi matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kieletroniki (NeST).
Kamishna wa Sera ya Ununuzi wa Umma, Dkt. Frederick Mwakibinga akiwasilisha Hotuba kwa wazabuni na Taasisi nunuzi kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Matumizi rasmi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko kieletroniki kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa tarehe 04 Februari 2025 jijini Mwanza.

Dkt. Mwigulu amezindua rasmi matumizi ya moduli hiyo Jijini Mwanza wakati wa mafunzo ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa (Complaint and Appeal Management Module) katika Mfumo wa NeST.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Kamishna wa Sera ya Ununuzi wa Umma, Dkt. Frederick Mwakibinga amesema kuwa kuanza rasmi kwa matumizi ya moduli kuna faida kadhaa zikiwemo kuokoa muda, gharama, kupunguza mianya ya rushwa, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ununuzi wa Umma.

“Moduli hii mpya inalenga kurahisisha zoezi zima la uwasilishaji wa malalamiko na rufaa kwa upande wa wazabuni na pia itawezesha taasisi nunuzi na Mamlaka ya Rufani kushughulikia Malalamiko na rufaa kupitia Moduli hii hivyo kupunguza muda na gharama zinazo ambatana na zoezi zima la utoaji wa haki,” amesema Dkt. Mwigulu.
Dkt. Mwigulu alitoa rai kwa wazabuni wote nchini pamoja na taasisi nunuzi kuwa tayari kujifunza na kutumia Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki ili kuokoa muda na fedha ambazo zingetumika katika uwasilishaji na ushughulikiaji malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa Umma.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Bw. James Sando amesema kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi Imara wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, PPAA imeweza kushughulikia mashauri 162 yaliyotokana na michakato mbalimbali ya Ununuzi wa Umma.
Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) Bw. James Sando akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi rasmi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kieletroniki kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa tarehe 04 Februari 2025 jijini Mwanza.

“Katika mashauri hayo, PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 35 zenye thamani ya takriban shilingi bilioni 583.6 kwa wazabuni wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika, amesema Bw. Sando.

Bw. Sando aliongeza kitendo cha kuzuia tuzo kwa wazabuni hao kiliiepusha Serikali kuingia katika mikataba ambayo ingepelekea kuwa na utekelezaji wa miradi usioridhisha hivyo kusababisha upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo stahiki kwa wananchi.

“PPAA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi zinazosimamia ununuzi wa Umma nchini, imeweza kushiriki katika kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024,"amesema Bw. Sando.

Bw. Sando ameongeza kuwa, ili kuendana na mabadiliko yaliyoletwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma, PPAA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi zinazosimamia ununuzi wa Umma nchini, imeandaa Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024 ambazo zimetangazwa kwenye Gazeti la tarehe 31/01/2025 kupitia Gazeti la Serikali (GN no.65/2025).
Mafunzo ya matumizi rasmi ya moduli awamu ya pili kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa yametanguliwa na mafunzo ya awamu ya kwanza yaliyofanyika Mwezi Mei 2024 kwa mikoa ya kanda ya Pwani iliyojumuisha Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news