Waziri Kombo ateta na wanafunzi wa Chuo cha Diplomasia Hungary

BUDEPAST-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ametembelea Chuo cha Diplomasia cha Hungary na kutoa mhadhara kwa wanafunzi wa Chuo hicho kuhusu Sera ya Mambo ya Nje na mchango wa Tanzania katika kutatua changamoto mtambuka ulimwenguni ikiwemo ulinzi na usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu, mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira.
Akizungumza katika mhadhara huo, Mhe. Waziri Kombo ameeleza historia ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ambayo ililenga kusaidia ukombizi wa nchi za kusini mwa Afrika.

Ameongeza kuwa kwa sasa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania imejikita kutekeleza Diplomasia ya Uchumi inayolenga kuvutia manufaa ya kiuchumi kwa kukuza biashara, uwekezaji na Utalii na nchi marafiki na hivyo kukuza uchumi wa nchi.
Kuhusu mchango wa Tanzania katika kutatua changamoto mbalimbali duniani, Mhe. Waziri Kombo amesema chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imetoa kipaumbele kutatua changamoto za amani na usalama barani Afrika ambapo hivi karibuni ilikua mwenyeji wa Mkutano wa pamoja wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya za SADC na EAC ambacho kililenga kutafuta suluhisho la kudumu kwa amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa upande wa mazingira, Mhe. Kombo ameeleza jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, programu ambayo imeungwa mkono ulimwenguni na wadau mbalimbali ikiwemo Umoja wa Afrika, Nchi za G20, SADC na EAC.
Aidha, ameeleze kitendo cha hivi karibuni ambapo Tanzania ilikua mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliowaleta pamoja viongozi wa Afrika kujadili namna ya kusambaza kwa watu milioni 300 nishati safi ya umeme ifikapo mwaka 2030.Waziri Kombo alihitimisha muhadhara huo kwa kuwaalika wanafunzi hao kutembelea Tanzania ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na kuimarisha ushirikiano na mwingiliano wa watu kwa watu kati ya Tanzania na Hungary.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news