DODOMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu),Mhe. William Lukuvi ameelekeza Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kujiratibu vizuri katika kufikisha taarifa zote za taadhari ya maafa kwa wakati ili utekelezaji wake ufanyike mapema kabla ya madhara kutokea.
Kauli hiyo ametoa leo Februari 26,2025 alipotembelea Kituo cha Ufuatiliaji wa Majanga Katika Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
"Kwa nafasi mliyonayo na teknolojia mnazotumia mnaweza kujua na kutoa taarifa zote za tahadhari bila urasimu, ili kuepuka athari kubwa za maafa zinazoweza kutokea baadae."
"Aidha, muangalie na uwezekano wa kurahisisha mawasialiano ya taarifa zote za tahadhari ziweze kupatikana kila siku kwa njia ya simu ili kila mtu anayeenda kwenye shughuli ajue na achukue tahadhari.
“Huduma hii iwe bure na ipatikane muda wote ili wananchi waingie wasome na wachukue tahadhari, na tutakuwa tumefanya kazi yetu vyema,” amesema.

Amefafanua kwamba katika Ngazi ya Mikoa kuna vituo vya maafa vinapaswa kuanzishwa na jukumu hilo limeainishwa katika sheria ya maafa ya mwaka 2022 ambayo imeeleza kila Mkoa, kuwa na kituo cha usimamizi wa maafa ili kufanya ufuatiliaji wa majanga yanayoweza kutokea katika eneo la Mkoa husika.
Hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu inafanya ufuatiliaji wa uanzishwaji wa vituo hivyo ambapo wameweza kukutana na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa ambao kisheria wamepewa jukumu la usimamizi wa vituo hivyo ili kujengeana uelewa wa miongozo na namna ya uanzishaji na usimamizi wa vituo hivyo.
“Vituo hivyo vya Mikoa vitaunganishwa na mifumo ya Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ili waweze kufanya ufuatiliaji kwa karibu,” alibainisha Bi. Jane.