Waziri Mchengerwa atoa maagizo kuhusu NeST

DODOMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa amezitaka ofisi za sekretariati za mikoa nchini, wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za mitaa zote na maafisa ununuzi kuzingatia takwa la kisheria la ununuzi kufanyika kwa njia ya Mfumo wa Ununuzi wa Ununuzi wa Umma wa Kielektroniki (NeST).
Pia, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kusimamia sheria kwa kuhakikisha taasisi nunuzi zotezinafanya ununuzi kwa kutumia NeST.

Waziri Mchengerwa ameyasema hayo Februari 4,2025 jijini katika kikao kazi cha viongozi kutoka OR-TAMISEMI, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Makatibu Tawala Wasaidizi (Miundombinu),Maafisa Manunuzi wa Mikoa,Wakurugenzi na Maafisa Manunuzi wa MSM.

Kikao kazi hicho kimeangazia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.10 ya mwaka 2023 na matumizi ya Mfumo wa Ununuzi wa Ununuzi wa Umma wa Kielektroniki (NEST) katika Ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.

"Kama tunavyofahamu, tarehe 29/9/2023 Mheshimiwa Rais alisaini Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma na hivyo kurasimisha kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.10 ya Mwaka 2023.

"Aidha,Mheshimiwa Rais ameendelea kutoa maelekezo mahsusi ya kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa katika matumizi ya fedha za umma katika miradi mbalimbali."

Waziri Mchengerwa amesema, eneo hilo linalotumia fedha nyingi sana, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha zinatumika ipasavyo, kwani asilimia 70 ya bajeti ya Serikali inakwenda katika ununuzi wa umma.

"Chukueni hatua kwa wanaokiuka takwa hili la kisheria,kwani iko wazi hatua za kuchukua juu ya ukiukwaji wautaratibu huu.

"Naelekeza kuhakikisha miradi yote inakuwa na thamaniya fedha na inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa."

Waziri Mchengerwa amesema,kama kuna changamoto yoyote wawasiliane na PPRA kwani wapo tayari kutatua changamoto zozote zinazoweza kujitokeza.

Vilevile amesema,wanaendelea kuchukua hatua kwa wale wasiozingatia thamani ya fedha na kuruhusu vitendo vya ubadhirifu wa fedha ya umma kuendelea.

"Nawaelekeza kuzingatia takwa la kutenga bajeti ya ununuzi kwa makundi maalum kama inavyoelekezwa na sheria.

"Nasisitiza jambo hili lipewe umuhimu unaostahili. Nawaelekeza kusimamia fedha nyingi ambazo Serikali imetenga na kuleta katika maeneo yenu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

"Niliwahi kusema na nasisitiza hapa Mkurugenzi kushindwa kutekeleza miradi kwa wakati inawanyima haki wananchi kutumia miradi hiyo. Nasisitiza hili halikubaliki. Kila mmojaatimize wajibu wake,"amesisitiza Waziri Mchengerwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news