SHINYANGA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemtaka mkandarasi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga afanye kazi usiku na mchana ili kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa uwanja huo ikiwemo ufungaji wa taa na uanze kutumika wakati wote.
Amesema kuwa uwanja huo niwa kimkakati uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu na wakazi wa mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani ikiwemo mkoa wa Simiyu.
Amesema hayo leo Jumapili ya Februari 16, 2025 wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga ambao kwa ujumla ujenzi wake umefikia Asilimia 73.9.

Amesema kuwa dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha Sekta ya usafirishaji ni dhamira kamili na kwasasa inatekelezwa kwa vitendo.
“Leo hii kila mkoa tuna uwanja wa ndege ukiondoa mikoa mipya ikiwemo Simiyu lakini Serikali inaendelea na ujenzi katika maeneo hayo.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania waliofanya kazi za ujenzi kwenye uwanja wa ndege wa Shinyanga kutumia uzoefu na ujuzi walioupata kujiendeleza na ikiwezekana kuanzisha makampuni ya ujenzi ili kunufaika na miradi mingine itakayotolewa na Serikali.
Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa huo ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege.

Kwa upande wake Meneja wa TANROAD mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samwel Mwambungu Amesema kuwa Serikali katika kuhakikisha inaendelea kuboresha usafiri wa anga kwa mkoa wa Shinyanga, iliingia mkataba na mkandarasi kutoka China (CHICO) kwa gharama ya Shilingi bilioni 49.2 kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga.

Maeneo mengine ni usimikaji wa taa za kuongozea ndege, ujenzi wa mitaro ya maji, uzio kuzunguka kiwanja, barabara ya mzunguko ndani ya kiwanja na barabara za kufikia kwenye uwanja wa ndege.