Waziri Mkuu azitaka mamlaka za mikoa na taasisi za elimu kusimamia utekelezaji Sera ya Elimu

DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka za mikoa, halmashauri na taasisi za elimu nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la mwaka 2023, kwa ufanisi kulingana na majukumu yao.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka halmashauri ziweke kipaumbele katika kuanzisha na kuendesha shule za amali ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri na hatimaye kuchangia katika maendeleo ya Taifa letu.

Ametoa maelekezo hayo leo Februari 14, 2025 wakati akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 18 wa Bunge la 12, bungeni jijini Dodoma.

“Sera na Mitaala hiyo ni maono na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kufanya elimu inayotolewa hapa nchini iwiane na mahitaji ya sasa, lakini pia wahitimu wapate stadi na maarifa yatakayomudu mabadiliko na kasi ya ukuaji wa teknolojia”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini imeendelea kuimarika ambapo katika msimu wa 2023/2024 uzalishaji wa mazao ya chakula ulifikia tani milioni 22.8.

“Kwa kuzingatia uzalishaji huo na mahitaji ya chakula ya tani milioni 17.7 kwa mwaka 2024/2025, nchi itakuwa na utoshelevu wa asilimia 128.

"Hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2025 Wakala imehifadhi jumla ya tani 776,000 za nafaka katika ghala za Wakala zilizopo kwenye maeneo mbalimbali nchini.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi wanaoishi kwenye baadhi ya maeneo nchini yanayopata mvua chache kuchukua tahadhari mapema na kuzalisha mazao yanayokomaa kwa muda mfupi.

“Hatua hii iende sambamba na kutumia vizuri mavuno yaliyopatikana kwa kutunza chakula cha kutosha katika ngazi ya kaya”

Akizungumzia kuhusu tuzo maalum ya Kimataifa ya The Global Goalkeeper Award aliyopewa Rais Dkt. Samia kutoka Taasisi ya Gates, Mheshimiwa Majaliwa amesema tuzo hiyo ni kielelezo cha utashi wake katika kuharakisha malengo ya maendeleo endelevu nchini.
Pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amepewa tuzo hiyo kutokana na jitihada alizozifanya katika kupunguza viwango vya vifo vya wajawazito na watoto chini miaka mitano lakini pia kukabiliana na tatizo la udumavu”

Mheshimiwa Majaliwa amesema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kiwango cha vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua kutoka vifo 556 mwaka 2015 hadi vifo 104 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 100,000. Idadi hiyo nisawa na asilimia 80.”

Pia, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa rai kwa wafanyabiashara wote kutopandisha bei za vyakula kiholela wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

“Wafanyabiashara wote watambue ya kwamba mchango wao ni muhimu katika kufanikisha ibada hii, ninawasihi sana endeleeni kushiriki katika ibada hii kwa kurahisisha upatikanaji wa bidhaa muhimu”. Bunge limeahirishwa hadi siku ya Jumanne Aprili 08, 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news