Wizara ya Fedha yafikisha Elimu ya Fedha wilayani Siha

NA EVA NGOWI
WF Kilimanjaro

WIZARA ya Fedha kupitia Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha imewajengea uelewa wa Elimu ya Fedha Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Wanavikundi na Wajasiriamali wadogo wadogo walioshiriki katika semina zinazoendelea katika Kata, Wilaya mbalimbali Mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Bw. Haji Mnasi, akimsikiliza Afisa Mkuu Mwanadamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, kuhusu elimu ya fedha kabla ya kuanza kwa semina kwa watumishi wa Halmashauri hiyo.

Semina hiyo ya Elimu ya Fedha iliyotolewa kwa Watumishi ilifanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, na kwa Wanavikundi na Wajasiriamali wadogo wadogo ilifanyika katika Ukumbi wa Family Conference Hall na Ofisi ya Tarafa ya Siha Kati, Kata ya Fuka Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Bw. Haji Mnasi, akizungumza na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha (hawaonekani pichani) wakiwa ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa Elimu ya Fedha kwa Watumishi wa Halmashauri hiyo.

Akiikaribisha Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Bw. Haji Mnasi, alisema kuwa amefurahishwa na ujio wa Timu hiyo kuja kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya Uwekaji Akiba, Mikopo na Uwekezaji kwani ni fursa kubwa kwa watumishi wa Halmashauri yake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Bw. Haji Mnasi, akizungumza na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, wakiwa ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa Elimu ya Fedha kwa Watumishi wa Halmashauri hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya Elimu ya Fedha kwa Watumishi wa Halmashauri ya Siha Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, alisema ni vyema watumishi wa umma wakatumia elimu hiyo ya fedha ili kuboresha matumizi yao ya kila siku na kuweka akiba ili kuepuka kuchukua mikopo kausha damu.
Afisa Mkuu Mwanadamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, akitoa elimu ya fedha kwa Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Afisa Usimamizi Fedha Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Jackson Mshumba, akitoa elimu ya fedha kwa Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.

“Elimu hii itawawezesha kufahamu ni wakati gani unatakiwa kuchukua mkopo na namna bora ya kuutumia, pia itawawezesha kufahamu mahali salama kwa kuwekeza fedha kidogo kidogo ili kuboresha hali ya uchumi na kuwaondolea mawazo ya kukopa kila wakati.” Alisema Bw. Kimaro.

Aidha, Afisa Mwandamizi Masoko na Mawasiliano kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, aliwahimizi Watumishi wa Umma, Wanavikundi na Wajasiriamali wadogo wadogo kujijengea utamaduni wa kuweka akiba kila wanapopata kipato ili iwasaidie kuwaongezea katika uwekezaji na kukuza uchumi.
Afisa Mwandamizi Masoko na Mawasiliano, kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akitoa elimu ya uwekezaji kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro.
Diwani wa Kata ya Kirua, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Bw. Samuel Emmanuel Mmaru (kulia), akibadilishana mawazo na Afisa Mkuu Mwanadamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, wakati wa Semina ya Elimu ya Fedha iliyofanyika katika Ukumbi wa Family Conference Hall, Kata ya Fuka, Wilaya ya Siha, Mkoani Kilimanjaro.

Bw. Mwanga alisema kuwa ili kuweka akiba ya fedha ni vyema wakabainisha matumizi yasiyo ya lazima na kuyaondoa na kufanya akiba kuwa ni sehemu ya matumizi ya lazima kila wanapopata fedha.

“Ukiwa na utamaduni wa kuweka akiba, suala la kuwekeza fedha linakuwa ni rahisi, na unaweza ukawekeza kwenye kilimo, biashara, na Masoko ya Mitaji ikiwemo Hisa na Hati Fungani ili kuiwezesha akiba yako unayoitunza kukua na kuongezeka” Alifafanua Bw. Mwanga.

Katika kuhitimisha semina ya Elimu ya Fedha kwa Watumishi, Wajasiriamali na Wanavikundi, Afisa Usimamizi Fedha Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Bw. Jackson Mshumba, alisema kuwa Serikali inajua kuwa kuna changamoto kubwa zinazotokana na uelewa mdogo wa elimu ya fedha hasa katika masuala ya mikopo kuwa na riba kubwa na kusababisha migogoro kwenye familia mara mikopo hiyo inaposhindwa kulipika.
Diwani wa Kata ya Kirua, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Bw. Samuel Emmanuel Mmaru akiongea na baadhi ya Machinga, Wakulima, BodaBoda, Mama/ Baba Lishe na Vikundi vya Huduma ndogo za Fedha kuhusu ushiriki wa semina za elimu ya fedha zinazoendelea Mkoani Kilimanjaro.
Wananchi wakifuatilia filamu ya Elimu ya Fedha (haionekani pichani) iliyokuwa ikioneshwa katika Ofisi ya Tarafa ya Siha, Kati Kata ya Kirua, Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya wakinamama wajasiriamali kutoka katika kikundi cha Changamkeni Women Group wakiwa katika picha ya pamoja na kuonesha baadhi ya bidhaa wanazozitengeneza.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Kilimanjaro).

“Tunawaomba watumishi na wananchi kwa ujumla watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa mara tu wanapobaini kuwa kuna watoa huduma za fedha ambao wanakiuka utaratibu wa kisheria ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria,” asema Bw. Mshumba.

Semina ya Elimu ya Fedha imetolewa wilayani Siha mkoani Kilimanjaro kwa Machinga, Wakulima, BodaBoda, Mama/ Baba Lishe na Vikundi vya Huduma ndogo za Fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news