NA DIRAMAKINI
YOUNG Africans Sports Club (Yanga SC) imerejea kwa kishindo michuano ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya kuishindilia Kagera Sugar mabao 4-0.
Ni kupitia mtanange uliopigwa leo Februari 1,2025 katika Dimba la KMC Complex lililopo Mwenge katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga yamefungwa na Clement Mzize dakika ya 32,Mudathir Yahya dakika ya 60, huku Pacôme Zouzoua akipachika bao la tatu kwa mkwaju wa penalti dakika ya 78. Bao la nne limefungwa na Kennedy Musonda dakika ya 86.
Kwa sasa Young Africans Sports Club inafikisha alama 42 baada ya mechi 16 za Ligi Kuu ya NBS Tanzania Bara ikiwa ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Aidha, katika msimamo wa Ligi Kuu hiyo, nafasi ya pili inashikiliwa na Simba Sports Club yenye alama 40 baada ya mechi 15.
Vilevile, nafasi ya tatu inashikiliwa na Azam FC yenye alama 36 baada ya mechi 16, nafasi ya nne inashikiliwa na Singida Black Stars yenye alama 33 baada ya mechi 16.
Tabora United FC ambayo inatajwa kuwa gumzo na kisiki kwa wakongwe wa ligi hiyo inashika nafasi ya tano kwa alama 25 baada ya mechi 15.
Mbali na hayo,Kagera Sugar wanasalia nafasi ya pili kutoka mkiani wakiwa na alama 11 baada ya mechi 16 za ligi hiyo yenye ushindani mkubwa.