NA DIRAMAKINI
MABINGWA wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Young Africans Sports Club (Yanga SC) ya jijini Dar es Salaam imetinga katika kilele cha msimamo wa ligi hiyo kwa kishindo baada ya kuichapa Ken Gold FC mabao 6-1.
Yanga SC imepata ushindi huo mnono leo Februari 5,2025 katika dimba la KMC Complex lililopo Mwenge katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Katika mtanange huo,pia Clement Mzize amekwea kileleni mwa mbio za ufungaji bora baada ya kufikisha magoli tisa.
Dakika ya pili ya kipindi cha kwanza cha mtanange huo,Yanga SC ilianza kurekodi bao la kwanza kupitia kwa Prince Dube huku dakika ya sita Clement Mzize akipachika bao la pili.
Pacôme Zouzoua dakika ya 39 aliongeza bao la tatu kwa Yanga SC ambapo kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika dakika ya 43, Mzize alirejea tena nyavuni kwa bao la nne.
Aidha, Dube dakika ya 46 alifunga bao la tano na dakika ya 85, Duke Abuya alifunga bao la sita huku Ken Gold FC wakipata bao la kufuta machozi kutoka kwa Seleman Bwenzi dakika ya 86.
KenGold FC kwa matokeo haya, jahazi linazidi kuzama kwani bado wanashikilia mkia kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama sita pekee baada ya michezo 17.
Pia,leo wamekutana na Yanga SC wakiwa na rekodi mbaya ya kufungwa mechi nne mfululizo, jambo linalowafanya kuwa katika hatari kubwa ya kushuka daraja kwa sasa.
Awali, KenGold walijaribu kuimarisha kikosi chao katika dirisha dogo la usajili kwa kufanya mabadiliko makubwa, wakisajili wachezaji wazoefu kama Bernard Morrison aliyewahi kuchezea Yanga na Simba, Obrey Chirwa, Zawadi Mauya, na Kelvin Yondani.
KenGold pia walifanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwa kumleta kocha mpya, Vladislav Heric, ambaye ni kocha wao wa nne msimu huu.
Yanga SC kwa matokeo ya leo inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwa alama 45 baada ya mechi 17 huku nafasi ya pili ikishililiwa na watani zao Simba SC kwa alama 43 baada ya mechi 16.
Chini ni msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya mechi za leo Februari 5,2025;