ZANZIBAR-Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mheshimiwa Mudrik Ramadhan Soraga amewataka wasanii na wananchi wa Zanzibar kutumia fursa ya Tamasha la Trace Music Award ili kuweza kuviendeleza vipaji vyao.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali katika Hotel ya Verde Mtoni Mkoa wa Mjini Unguja ambapo amesema, kufanyika kwa tamasha hilo hapa Zanzibar litasaidia kuwaendeleza wasanii mbalimbali katika nyanja tofauti.
Mheshimiwa Soraga ameeleza kuwa, kupitia tamasha hilo kutakuwa na utoaji wa elimu husiana na kazi zinazofanywa na wasanii ili kutambua haki zao kupitia sanaa zao kwani baadhi ya wasanii hawafahamu vizuri majukumu yao, hivyo wanashindwa kufikia malengo waliyojiwekea kuutokana na changamoto mbalimbali.
Hata hivyo amefahamisha kuwa,tamasha hilo litaleta fursa ya kuutangaza utalii ndani ya Zanzibar ili kuimarisha uchumi wa nchi na kuleta maendeleo kwa taifa.
Waziri Soraga amesema zaidi ya watu 1,500 na washiriki 300 watahudhuria na kuwasisitiza wananchi kuchamkia fursa hiyo kwa kuuza biashara mbalimbali na kuutangaza utalii wa ndani katika kipindi cha tamasha ili kuwavutia watalii na kutajika zaidi.
Kwa upande wake CEO, Trace Music Award Oliver Lauouchez amesema tamasha hilo ni la pili kufanyika hapa Zanzibar ambalo linatarajiwa kuwashirikisha wasanii mbali mbali ikiwemo bongo fleva ili waendelee kujifunza na kujiendeleza katika fani zao.
Naye Msaidizi wa Jumuiya ya Uwakilishaji Watalii Zanzibar Wilsred Shirma amewataka wafanyabiashara, wakuu wa Makampuni kudhamini na kushiriki katika tunzo hizo na kutoa hamasa kwa wasanii kujitokeza kwa wingi ili wapate kujitangaza wao pamoja na kazi zao.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Februari 24, 25 na 26,mwaka huu katika Hoteli ya THE MORA Matemwe na kushirikisha wasanii mbalimbali barani Afrika na kwa upande wa Bongo fleva wasanii watakaoshiriki ni pamoja na Zuchu, Diamond na Hamonize na kurushwa na Chaneli zaidi ya 74 Kati ya hizo ikiwemo CNN.