ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema,Zanzibar itaendelea kuimarisha ushirikiano na Romania katika nyanja mbalimbali za maendeleo na kiuchumi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amemuelezea Balozi Gentiana kuwa yapo maeneo mengi ambayo pande hizo zinaweza kushirikiana ikiwemo Elimu , Afya, Mafuta na Gesi , Usimamizi wa Maafa na Udhibiti wa Taka Kitaalamu pamoja na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Akizungumzia suala la Mazingira Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa Zanzibar inakabiliwa na tatizo kubwa la Taka za plastiki zinazotishia Uhai wa Viumbe vya Baharini na Ustawi wa Sekta ya Utalii na kuiomba Romania kulizingatia eneo hilo.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amevikaribisha Vyuo Vikuu vya Romania kuja nchini kuangalia maeneo ya Ushirikiano na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).
Vilevile ametumia fursa hiyo kuwakaribisha Wawekezaji na Wafanyabiashara wa Romania kuja kuangalia fursa za Uwekezaji Hapa nchini.
Naye Balozi Gentiana Serbu ameihakikishia Zanzibar kuwa nchi hiyo itaendelea Kushirikiana nayo na kutoa Misaada katika sekta mbalimbali kwa lengo la kuleta Maendeleo na Ustawi wa Watu wake.