ZANZIBAR-Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma sawa za afya bila ubaguzi.
Akizungumza kabla ya kuzindua usajili wa sekta isiyo rasmi na makundi yaliobakia katika Mfuko wa Huduma za Afya (ZHSF), hafla iliyofanyika Darajani Souk Mjini Unguja alisisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuchangia katika mfuko huo ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wote.
Alisema mfuko huo ulianza kusajili watumishi wa umma na watendaji wa sekta binafsi mwaka 2023 ambao wameanza kunufaika na sasa unahusisha makundi mengine ikiwemo wageni wanaoishi Zanzibar kwa zaidi ya miezi sita, wastaafu, wanafunzi wa vyuo au Taasisi za Elimu ya juu, Wajasiriamali, wafanya biashara wakubwa na wadogo na wakazi wote wa Zanzibar ili nao wapate huduma za afya kupitia mfuko huo.
Aidha,Mazrui aliyataka makundi hayo kujisajili na kuchangia ili kuwekeza kwa mustakabali wa afya zao.
“Kujisajili na kuchangia kunalenga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa mwanachama na kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote na eneo lolote pamoja na kuufanya mfuko kumudu gharama za matibabu ya afya pale dharura ya maradhi inapotokea,” alifahamisha Mazrui.
Mbali na hayo Mazrui aliwashukuru washirika wa maendeleo wanaendelea kuungamkono jitihada hizo kwa kutoa msaada wa ushauri na uwezeshaji ikiwemo shirika la GIZ na D tree.
Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Huduma za Afya (ZHSF), Yaasin Ameir Juma, alisisitiza kuwa mfumo wa usajili umeimarishwa na kuwa unakidhi haja ya kukamilisha usajili wa makundi yote yaliyobakia baada ya kukamilisha zoezi la usajili wa watumishi wa umma na sekta binafsi na wategemezi wao.
Kuelekea zoezi hilo Yaasin aliwataka wananchi kutoa taarifa sahihi za kipato chao ili kila mmoja achangie kulingana na uwezo wake na kuupunguzia gharama mfuko huo uliyobeba wategemezi wengi ikiwemo watoto wa kuzaa ambao hawana ukomo.
Washirika wa maendeleo walisema suala la afya ni mtambuka na lenye kubebba uti wa mgongo wa uchumi na kusema kuwa mfuko huo ni tunu inayohitaji kuenziwa na umuhimu huja pale unapohitaji matibabu.