ATCL yaja na ofa ya kuwajaza fedha wateja wake

DAR-Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imetangaza zawadi kwa wateja wake katika msimu wa Sikukuu ya Eid na Pasaka, ikiwa ni ishara ya kusherehekea na wateja wao waaminifu.
Kwa mujibu wa ATCL,wateja watakaonunua tiketi za safari za kwenda Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) au maeneo mengine kupitia App ya ATCL au tovuti yao rasmi, watapata zawadi ya punguzo la hadi USD 50 kwa kila tiketi, kulingana na masharti ya safari husika.

“Tumeamua kuwashukuru wateja wetu kwa uaminifu wao kwa Air Tanzania kwa kuwarudishia hadi USD 50 msimu huu wa Eid na Pasaka,” amesema Sarah Reuben, Meneja Uhusiano na Mawasiliano ATCL.

Kwa upande wa safari za Kinshasa, ATCL itafanya safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Kinshasa, ambapo safari zitafanyika mara nne kwa wiki kwa siku ya Jumapili, Jumatatu, Jumatano na Ijumaa na zitafanyika asubuhi au mchana.

Kabla ya uzinduzi wa huduma hii, abiria walilazimika kutumia zaidi ya masaa nane kupitia nchi nyingine lakini lakini sasa watatumia chini ya masaa manne kufika Kinshasa kwa nauli ya kuanzia USD 372 kwa safari ya kwenda na kurudi.

Ofa hii, itakayodumu kwa takriban miezi miwili, ni fursa kwa Watanzania ambao sasa hawahitaji visa kusafiri kwenda DRC.

Kuanzishwa kwa safari za Kinshasa kunafanya ATCL kuwa na vituo viwili nchini DRC, baada ya Lubumbashi, hatua ambayo itamarisha mtandao wake wa safari na kuleta ushindani dhidi ya mashirika mengine ya ndege yanayohudumu eneo hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news