BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Arusha, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wafanyakazi wa Benki Kuu, wakiongozwa na Gavana Bw. Emmanuel Tutuba na Naibu Gavana Bi. Sauda Kassim Msemo, wamehudhuria na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maadhimisho hayo.
Pia, katika kuadhimisha siku hii, BoT imeendesha mafunzo maalum ya elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali ya wanawake wajasiriamali na wafanyabiashara jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wanawake kuelewa masuala muhimu ya kifedha, ikiwa ni pamoja na uwekezaji, namna Benki Kuu inavyolinda watumiaji wa huduma za kifedha, mifumo ya malipo, elimu sahihi ya mikopo, uchumi na masuala mengine muhimu ya fedha.
Washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Benki Kuu kwa kuwapatia fursa hiyo na kuomba ushirikiano zaidi ili waweze kupata mwongozo sahihi wa masuala ya kifedha.
Aidha, wameiomba BoT kufuatilia kwa karibu taasisi na watu wanaotoa mikopo nchini ili kuhakikisha wanafuata taratibu sahihi na hawawaumizi wananchi kwa masharti magumu ya mikopo.
Mafunzo haya yamewakutanisha zaidi ya wanawake 100 kutoka vikundi vya wajasiriamali vya Bunju Women Empowerment, Elite Ladies, na The Registered Trustees of Tanzania Community Empowerment Association, ambavyo vinajihusisha na biashara, ufugaji na shughuli nyingine za kiuchumi.