DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeuza kwa mnada dola za Marekani milioni 30 katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni (IFEM).
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Machi 18,2025 na Kurugenzi ya Masoko ya Fedha ya BoT.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, BoT imeshiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni ikiwa ni kwa mujibu wa sera yake ya ushiriki katika soko la fedha za kigeni ya mwaka 2023.
“Katika ushiriki huu, Benki Kuu imeuza Dola za Marekani milioni 30 kupitia mnada wa ushindani kwa kiwango cha wastani cha kubadilisha fedha za kigeni cha Sh. 2,646.00 kwa Dola moja ya Marekani,”imefafanua taarifa hiyo.
Aidha, imesema mnada ulifanyika kupitia mfumo wa kielekroniki wa kufanyia Minada ya Fedha za Kigeni yaani FX Auction System.
Taarifa hiyo imeweka matokeo ya mnada huo kuwa ni kiasi kilichotangazwa Dola 20,000,000.00, maombi yaliyowasilishwa 43,750,000.00, kiasi kilichokubaliwa 30,000,000.00, kiwango cha wastani kilichokubaliwa 2,646.00, kiwango cha juu cha ushindani 2,695.00, kiwango cha chini cha ushindani 2,610.00.
Aidha, imesema kiwango cha juu kilichokubaliwa 2,695.00, kiwango cha chini kilichokubaliwa 2,630.00, huku idadi ya benki zilizoshiriki 18 na idadi ya benki zilizoshinda 12.