NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania imeueleza umma kwamba,taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Watanzania wanaoishi nchi za nje (Diaspora) wanashindwa kufungua akaunti za benki na kulazimika kufuata kadi zao hapa nchini, hazina ukweli.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 14,2025 na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba imebainisha kuwa, ufuatilia uliofanywa na Benki Kuu katika benki za hapa nchini umebaini kwamba, taratibu zilizopo kwa wateja wa Diaspora ni rafiki na za haraka.
Pia, ameeleza kuwa,katika kuhakikisha kuwa Diaspora wanapata huduma kwa wakati, benki husika zimefungua madawati mahsusi yakuwahudumia wateja hao na nyingine zimeanzisha vifurushi maalumu vya Diaspora.
"Katika ufunguaji wa akaunti za Diaspora wa Tanzania, mteja anatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au hati ya kusafiria."
Ameeleza kuwa,vitambulisho hivyo vinaweza kuwasilishwa kwenye dawati la benki husika au kutumwa kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
"Baada ya akaunti kufunguliwa, mteja ana uhuru wa kuchukua kadi yake mwenyewe kwa kwenda kwenye benki husika endapo yupo hapa nchini, au kuielekeza benki yake namna anavyotaka kutumiwa kadi hiyo ili imfikie mahali aliko.
"Kwa taarifa hii, Diaspora wa Tanzania wanahimizwa kuendelea kutumia benki zetu katika kupata huduma zao na hivyo kuchangia katika maendeleo na uchumi wa taifa letu.
"Aidha, benki za biashara zinahimizwa kuendelea kutoa elimu kuhusu huduma zao kwa wananchi wote,wakiwemo Diaspora wa Tanzania, ili waweze kujua taratibu zinazotakiwa kufuatwa, nyaraka za msingi, na kupatiwa huduma stahiki kwa wakati bila changamoto zozote."
Gavana Tutuba amebainisha kuwa,Benki Kuu inaunga mkono jitihada za Serikali za kuwahimiza Diaspora wa Tanzania kuwekeza nchini kwa ajili yao na maendeleo ya uchumi wa taifa letu.
"Hivyo, (Benki Kuu) itaendelea kufuatilia ili kuhakikisha endapo kuna mteja mwenye changamoto mahsusi kwenye benki yoyote, inatatuliwa na kumuwezesha kupata huduma za kibenki kwa ukamilifu na haraka."