BoT,wadau Sekta ya Fedha wajadili pengo la kijinsia katika huduma za fedha

DAR-Benki Kuu ya Tanzania imeendesha mkutano na viongozi mbalimbali wa sekta ya fedha, hususan sekta ya kibenki, pamoja na wadau wa maendeleo. Katika mkutano huo, wamejadili masuala mbalimbali yatakayosaidia kuziba pengo la kijinsia katika Huduma Jumuishi za Fedha nchini.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa Habari leo tarehe 5 Machi, 2025, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema utafiti wa Finscope wa mwaka 2023, unaonesha kuwa wanawake hawajafikiwa na wana matumizi madogo ya huduma rasmi za kifedha.

“Miongoni mwa kundi lililoonekana kutofikiwa vizuri na huduma rasmi za fedha ni Wanawake. Serikali na taasisi nyingine zinafanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha huduma rasmi za kifedha zinajumuisha watu wote hususani kundi la wanawake ambalo linaonekana limesahaulika.”
Ameongeza kuwa mkutano huo utajadili fursa zilizopo na namna ya kutumia fursa hizo katika kuziba pengo lililopo kati ya wanaume na wanawake katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha nchini.

Aidha, amesisitiza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoandaliwa kwa upande wa Tanzania Bara, zinatazamia kuwa na uwiano wa asilimia Hamsini (50) kwa Hamsini (50) kati ya wanawake na wanaume ifikapo 2033.

“Lengo hili limezingatia mazingira tuliyonayo nchini, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoandaliwa kwa upande wa Tanzania Bara pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa miaka 10 ambao ulianza kutekelezwa tangu 2020 ambazo zote zinajielekeza katika kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia watu wote nchini bila kujali tofauti zao za kijinsia kwa ajili ya kuwezesha ukuaji wa uchumi endelevu.”Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki, Bw. Theobald Sabi, amesisitiza kuwa mabenki yanaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwafikia wanawake wengi na biashara zinazomilikiwa na kundi hilo ili kufikia lengo la uwiano wa asilimia Hamsini (50) kwa Hamsini (50) kati ya wanaume na wanawake ifikapo 2033.
Amesema, hatua hizo ni pamoja na ubunifu unaofanywa na benki za biashara katika kutengeneza bidhaa na huduma za kibenki mahususi kwa ajili ya wanawake ili kuondoa madhila mbalimbali yanayowakumba ikiwemo ukosefu wa mikopo.

Kwa upande wake, Meneja wa Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (International Finance Corporation) kwa nchi za Tanzania, Rwanda na Uganda, Bi. Martine Valcin, amesema suala la ujumuishi wa kijinsia katika upatikanaji na utumiaji wa huduma rasmi za kifedha ni la kipaumbele kwa Benki ya Dunia kutokana na mchango wake katika kustawisha uchumi wa Tanzania na dunia kwa ujumla.
Naye, Kiongozi wa Mpango wa Kuwawezesha Wajasiriamali Wanawake (WE-FI), Bi. Wendy Teleki, ameeleza kuwa Makubaliano ya Mpango wa Kuwawezesha Wajasiriamali Wanawake (Women Entrepreneurs Finance Initiative Code) uliozinduliwa leo unalenga kuzikutanisha taasisi za fedha mbalimbali nchini ili ziingie kwenye makubaliano ya kuwawezesha kifedha wajasiriamali wanawake nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news