ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Zanzibar ina kila sababu ya kuimarisha ushirikiano na Cuba kutokana na mchango unaotolewa na nchi hiyo kwa maendeleo ya Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo alipozungumza na Rais wa Baraza la Taifa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Cuba, Esteban Lazo Hernandez na Ujumbe wake waliofika Ikulu Zanzibar.
Aidha,Rais Dkt.Mwinyi ameishukuru Cuba kwa misaada inayoendelea kuitoa kwa Zanzibar, kwani imekua ikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo katika sekta tofauti hususan Sekta ya Afya na kuimarisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amesema,ujio wa ujumbe huo ni fursa muhimu ya kufungua maeneo mengine ya ushirikiano ikiwemo Uchumi wa Buluu, Elimu, Utalii, Teknolojia,Utamaduni na Michezo.